'Waliookoka wako kwenye vita kali’

Mwinjilisti wa Kanisa la Calvary Assemblies of God,   la Matarawe, Songea mkoani Ruvuma,  John Tembo, amewataka Wakristo waliofanikiwa kupata wokovu kutambua kuwa; wapo kwenye vita kali dhidi ya shetani, hivyo wanastahili kusimama imara nyakati hizi ni za mwisho.

 Wito huo alitowa mapema wiki jana, wakati akihubiri katika kanisa hilo, kwenye ibada ya Jumapili iliyokuwa na mguso mkubwa wa nguvu za Mungu, na watu zaidi ya 30 waliitikia wito wa Injili wakayakabidhi maisha yao kwa Yesu, huku waliosetwa na ibilisi wakifunguliwa.

 Mwinjilisti Tembo, alisema kuwa nyakati hizi ni za mwisho kwa mujibu wa maandiko, hivyo ni vema watu wakasimama imara kumuomba Mungu ili awaepushe na majaribu yanayowasonga.

 Alisema, watu wa Mungu waliouona mkono wa Bwana ndio waliopo kwenye changamoto mbalimbali za kishetani, kwa kuwa shetani naye anawatafuta watu kama hao ili awaangamize.

   “Nawaambieni watu wa Mungu katika nyakati hizi za mwisho shetani anafanya kazi ya kushika fahamu za watu wenye uelewa wa Mungu ili kusiwepo na utambuzi wa mambo mema, badala yake yatendeke mabaya,” alisema Mwinjilisti huyo na kuongeza:

 “Kuna baadhi ya watumishi wa Mungu wameshikwa ufahamu na shetani, na ninyi wenyewe mnaona, wanahubiria watu  vitu ambavyo havipo kwenye maandiko na mnamwamini,  ni hatari sana kwa nyakati hizi.”
 Aidha Mtumishi huyo wa Mungu aliwageukia waumini waliookoka ambao wamenunua simu kwa bei mbaya kwa malengo ya kuangalia picha za kishetani zilizopo ndani yake, na kulaani kitendo hicho kuwa ni kinyume na matumizi ya simu.

No comments:

Post a Comment