Chingafirst aja na mbinu mpya uimbaji nyimbo za injili

Kutokana na kukua kwa kasi kwa muziki wa Injili nchini, na kufanya miziki ya dunia kushuka katika tasnia ya muziki, mwimbaji William Chingafirst amekuja na staili mpya ya kumtukuza Mungu kwa njia ya uimbaji.
Mwimbaji Chingafirst, akiongea na chanzo ca blog jijini Dar es Salaam, alisema amekuja kivingine katika kumtukuza Mungu, pasi na ushindani, japo nyimbo zake zimeonekana kuleta ushindani maeneo ya Kahama, Geita na Tabora.

Akiongelea kuhusu albamu yake yenye nyimbo 11, alisema ameimba na kucheza kwa mitindo tofauti tofauti ikiwemo;  kwaito yenye asili ya Afrika Kusini, Rumba na Sebene toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, sambamba na Dansi asili yake Tanzania na nyimbo za kuabudu zenye mchanganyiko wa lugha ya kiingereza, kiswahili na kifaransa.

Alisema lengo lake ni kumwimbia Bwana kama ilivyo kule mbinguni ambapo malaika, wazee 24 na watakatifu wanavyomsifu Mungu kwa ukuu wake.

Aidha, aliongeza kuwa, yuko tayari kuimba kwenye kanisa lolote linalomhubiri Kristo aliye hai, linaloamini habari ya wokovu na tayari alishafanya katika baadhi ya makanisa jijini Dar es Salaam, akitamba na wimbo wa Sina Deni Aka Mie japo wimbo uliyobeba albamu yake ni Namshangilia Mwokozi.

Mwimbaji huyo anabainisha kuwa, uimbaji ni ibada tosha mbele za Mungu, huku akiongeza kuwa, Neno linahubiriwa kwa sababu watu wamemuacha Mungu, lakini kinachoendelea mbinguni katika ulimwengu wa roho ni sifa na kuabuudu.

Miongoni mwa nyimbo ndani ya albamu hiyo ni; Niko huru (mwanawane), This is the day you have made for me, Namshangilia Mwokozi, Ibelieve in You, Sina Deni Aka Mie, Tanzania Tunaweza kuuponya ulimwengu kwa jina la Yesu, Heri Wenye Moyo Safi, Twende kwa Bwana, Tutaimba Milele, Mtakatifu na Kila Jambo.
Alisema nyimbo hizo zimesanifiwa kiroho katika studio ya Hosana na maproduza tofauti tofauti.

No comments:

Post a Comment