Wafungwa wamsifu na kumuabudu Mungu

Waswahili husema historia hujirudia, hilo lilijidhihirisha hivi karibuni baada ya wafungwa wa gereza la vijana kusahau shida zao wakaruka ruka wakimsifu na kumuabudu Muumba wao kwa kicho na kububujika machozi, kama walivyofanya akina Paulo na Sila.

Hayo yalijitokeza hivi karibuni katika Kanisa la TAG Wami eneo la Gereza la vijana, Kilosa mkoani Morogoro, ambapo wafungwa walipata fursa ya kufika kwenye Ibada na kushiriki kikamilifu vipindi vyote, huku wakisindikizwa na Askari; ambapo pia walipewa nafasi ya kuimba nyimbo zilizosisimua waumini na kushangiliwa.

Miongoni mwa nyimbo zilizosisimua ni ile ya ‘Majaribu ni mtaji na wa kuinuliwa ni Mungu, wimbo uliowafanya baadhi ya washirika kusimama na kuanza kushangilia.

 Vijana hao walionekana kufunzwa vyema, kwani licha ya kuwa ni wafungwa, lakini walionyesha nidhamu ya hali ya juu wakati wote walipokuwa kwenye Ibada, kitu ambacho ni sehemu ya haki zao wapatazo wanapokuwa kifungoni.

Sula la wafungwa kumkumbuka Mungu wao na kuimba nyimbo za kuwatia moyo waumini linafananishwa na tendo la Mtume Paulo aliyeandika Nyaraka kadhaa akiwa gerezani za kuwapa moyo waumini waliokuwa wakipitia mateso mbalimbali.

Kadhalika wafungwa hao walipata fursa ya kusikiliza semina kuhusu Roho Mtakatifu, iliyoendeshwa na Walimu kutoka Kanisa la TAG Ubungo Christian Centre, la jijini Dar es Salaam, baadaye waliombewa ujazo wa Roho Mtakatifu pamoja na waumini wengine wa kanisa hilo.

Mchungaji Wilbald Ulomi, wa Kanisa hilo, mwisho wa ibada hiyo aliwashukuru wote waliohudhuria, ikiwa ni pamoja na walimu waliotoka Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment