Masikitiko ya mjane wa Mch. Kachila aliyeuwa kinyama katika mgogoro wa kuchinja

Katika mahojiano na Mwandishi wa Shirika la CBN News, mjane wa Mchungaji wa Kanisa la Kipentekoste aliyeuwa kinyama katika mgogoro wa kuchinja, Rev. Mathayo Kachila, Bi. Generosa Kachila, alitamka maneno yanayoashiria uchungu wa moyo wake kutokana na mkasa wenyewe na hata jinsi hatua za kisheria zilivyochukuliwa.

Kwa uchungu mama huyu alisema: "I shouted, my Jesus, my Jesus, why have you forsaken me?"  tafsiri isiyo rasmi “Nilipaza Yesu wangu Yesu wangu mbona umeniacha?” kilio hiki cha mshtuko wa kuuawa kwa mumewe aliyekuwa kiongozi wa familia, kumemuacha mjane huyu akiwa  mlezi pekee wa watoto 12.

Jambo baya zaidi ni kuwa mahojiano ya mama huyu yanaashiria uchungu zaidi kwa vile waliotekeleza  unyama huo hawajakamatwa na mwenyewe anaamini kuwa wako Mjini Mbeya na wengine  wamevuka mpaka na kuingia nchini  Burundi.

Ni wazi kuwa mjane huyo anaona jinsi juhudi zilivyofanyika kwa kuwatumia  wapelelezi wa kigeni kuwapata wauaji wa kasisi kule Zanzibar, kwa kuchorwa mchoro uliowezesha mtuhumiwa kukamatwa, na angependa kuwaona wahusika wa mkasa ule kuanzia wachochezi mpaka watekelezaji wakisimama mbele ya sheria.

Tunaamini kuwa  machozi ya mama huyu ni mashtaka mbele za Mungu ambaye Biblia inamuelezea kuwa ni baba wa yatima na Mume wa wajane.

Kwa kuwa yeye ndiye pia mhukumu Mkuu wa dunia  tuna hofu kuwa ikiwa tutazembea  kwa namna yoyote ile  kutenda haki iliyostahili, yaani kuwasaka wauaji wa mumewe kwa nguvu kubwa kama ile iliyotumika katika  matukio mengine yaliyoonekana ya muhimu.

Kwa mujibu wa utafiti wa Mwandishi wa CBN,  miongoni mwa watuhumiwa wakuu ni yule anayetajwa kwa jina moja la Abdallah ambaye inaelezwa kuwa yupo nchi jirani ya Burundi.

Tunaishauri serikali yetu kuimarisha msako wa watuhumiwa wote ili haki itendeke na wale waliopoteza mpendwa wao waione na kuitambua haki  hiyo.

Ni vyema pia serikali ikafahamu kuwa suala hili sasa lina sura ya kimataifa na ulimwengu unasubiri kusikia hatua madhubuti zinazochukuliwa katika kuilinda amani ya  nchi.Hatua hizo madhubuti zitafuata kile kilichoelezwa karibuni na mmoja wa wahubiri wa kimataifa kutoka  Ulaya kuwa mataifa ya magharibi yana kampeni maalumu ya kuionyesha dunia kuwa Tanzania si kisiwa cha amani tena.

Tunaamini kuwa haki ndiyo nguzo kuu ya amani yetu, tusipojali haki hata ya mnyonge  amani yetu itakuwa bandia au woga na wala si ile inayojengwa na nguzo ya upendo na undugu wa kweli.

Pia tunaishauri tena serikali kuliamua suala la uchinjaji ambalo ni chanzo cha  mauaji ya mchungaji huyo, liamuliwe kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi ambao ndio mkataba baina ya watawala na watawaliwa.
Wakati huu wa kusubiri serikali kuamua, pia wachungaji na viongozi wengine wa dini wajiapushe na lugha kali zinazoweza kuchochea chuki zaidi.

Wadumu katika kuomba, kushauri kwa upendo na kuelekeza kwa kuwa dunia inawatarajia kuwa waamuzi wakati mambo yanapoharibika.

Ni vyema watanzania nao wakajitambua  na kujitenga na watu wenye  nia mbaya wawe ni wa ndani au wa nje ya nchi wanaotaka kuona damu ya watu ikimwagika. Ni wazi kuwa kila mmoja wetu anajua kilichotokea katika mataifa jirani kuanzia, Rwanda, (mauaji ya kimbari 1994) Kenya ( mauaji ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007) na hata yale ya Burundi na Kongo.

No comments:

Post a Comment