Harris Kapiga: Mchungaji aliyefungua ‘klabu ya usiku’ Dar

Mchungaji Harris Kapiga
Imezoeleka kuwa klabu za usiku zimekuwa zikitumika kwa mambo ya starehe huku viongozi wa dini wakizichukulia kama maeneo hatari kwa waumini wao.

Tofauti na maeneo mengine ya starehe, klabu za usiku huwa na kumbi za muziki zenye taa za kumweka za rangi mbalimbali huku giza likitawala. Wakati huo huo muziku hupigwa kwa sauti ya juu.

Mbali na muziki, klabu hizo husheheni vileo vya kila aina huku watu wakiruhusiwa kuingia na mavazi yoyote wakiwemo wale wanaopenda kuvaa nuzu uchi.

Hata hivyo kwa watumishi wengine wa Mungu, klabu sasa ndiyo pamekuwa mahali pa kuvunia waumini.

Mchungaji Harris Kapiga wa kanisa la Nchi ya Ahadi lililoko Sinza Kamanyola, ameamua kuanzisha klabu ya usiku kama zilivyo klabu nyingine za starehe.

Klabu hiyo iliyozinduliwa hivi karibuni maeneo ya Mbezi Tangibovu katika hoteli inayoitwa Mak Hotel, imeonekana kuvutia vijana wengi ambao walionekana wakifurahia mandhari na muziki uliokuwa ukipigwa ndani yake.

Tofauti na klabu nyinginezo, Mchungaji Kapiga anasema kutakuwa na udhibiti wa vishawishi vya dhambi ikiwa pamoja na ulevi, mavazi yasiyo na staha na aina ya muziki unaopigwa.

Anasema tangu alipoanzisha wazo hilo, watu wengi hasa wachungaji walikuwa na wasiwasi kuhusu vishawishi hivyo.

“Tangu nimeanza wazo langu hili nimekumbana na vikwazo vingi. Imeshtua watu wengi, japo wengi wamelikubali na kuna baadhi hawakubali ila hawawezi kusema wazi,” anasema na kuongeza:

“Wengine wanajiuliza nitawezaje kudhibiti vipi hali ya klabu kwa sababu maeneo haya kunakuwa na anasa, ulevi na masuala ya mavazi watu watavaaje, na mimi nawajibu.”

“Mtu akija hapa na mavazi mabaya hataingia, tutakuwa makini sana katika hili. Mtu avae nguo yenye staha, siyo mtu aje nusu uchi, tutamtoa kwa nia njema tu. Hata mtu aliyelewa tutamtoa labda tusimgundue.”

Kwa nini ameanzisha klabu ya usiku? Mchungaji Kapiga anasema alianza kupata wazo hilo siku alipokuwa kwenye sherehe za kuadhimisha kuzaliwa kwa Clouds Media ambako pia ameajiriwa kama mtangazaji.


Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment