Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francisko atoa salamu za Mwaka Mpya

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Francisko
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Francisko ametoa ujumbe maalumu wa salamu za Mwaka Mpya, akisema vitendo vya rushwa na ufisadi ndivyo vinavyotishia kuuvuruga umoja na amani dunia.

Katika ujumbe huo alioutoa Makao Makuu ya Kanisa Katoliki mjini Vatican, Papa Francisko alilitaja tishio jingine la dunia ni uahalifu wa makundi.

“Rushwa na ufisadi pamoja na uhalifu wa makundi ni mambo yanayotishia udugu,” inaeleza sehemu ya ujumbe huo wa Papa, uliohaririwa na Padri Richard Mjigwa, wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Alitoa ujumbe huo wa mwaka mpya wakati Kanisa Katoliki duniani likiwa kwenye maombi kuomba amani duniani kwa siku  50, kwa kile kilichoelezwa kuenea kwa chuki, machafuko na kusababisha uhasama na vita sehemu nyingi.

Alisisitiza kuwa njia pekee ya kuvunjilia mbali uhalifu na vitendo hivyo viovu duniani ni jamii kuwa na moyo wa kuhurumiana na kujenga undugu.

“Udugu unavunjilia mbali ubinafsi ambao ni chanzo cha mifumo ya rushwa na ufisadi, uhalifu na uvunjifu wa utawala wa sheria,” alisema Papa Francisko.

Alisisitiza kuwa rushwa na ufisadi ni mambo ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kudhalilisha utu na heshima ya binadamu pamoja na mazingira.

No comments:

Post a Comment