Maaskofu: Watawala heshimuni maoni ya wananchi Katiba mpya

Maaskofu wa Makanisa mbalimbali mchini, wamezungumzia kwa nyakati tofauti mustakabali wa Taifa huku wakitaka watawala kuheshimu maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu Katiba mpya pamoja kuchukua hatua mapema kwa viongozi waliopewa dhamana za kuongoza na kushindwa kuwajibika.
 
Katika mahubiri yake kwenye Kanisa Kuu la Utatu Mtakatifu, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Morogoro, Godfrey Seheba, alitaka watawala kuheshimu mapendekezo yote yalitolewa katika rasimu ya pili ya Katiba iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba.
 
Askofu Seheba alisema kuwa mapendekezo hayo yaliyotolewa na wananchi iwapo yataheshimiwa na kupitishwa katika Bunge la Katiba, yatasaidia kuleta umoja na mshikamano ili kuifanya nchi kuwa na amani na utulivu kama ilivyokuwa na sifa yake.
 
Hata hivyo, Askofu Seheba alisisitizia umuhimu wa Watanzania kuendelea kuombea rasimu hiyo ili ipatikane kwa Katiba mpya itakayokidhi mahitaji ya Watanzania kwa maslahi ya nchi na ustawi wa jamii.
 
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheri la Kiinjili Jimbo la Morogoro, Jacob Mameo, akizungumza katika mahubiri yake katika Kanisa la Mji mpya, alisema mwaka 2014, uwe ni mwaka wa serikali kuchukua hatua za haraka kwa viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza na kushindwa kuwajibika badala ya kusubiri madhara kujitokeza kwa wananchi.
 
Askofu Mameo alisema mwishoni mwa mwaka jana, Taifa lilishuhudia madhara makubwa waliyopata wananchi wakati wa Operesheni Tokemeza kutokana na viongozi hao waliopewa mamlaka kushindwa kusimamia ipasavyo.
 
Alisema hali hiyo isipodhibitiwa mapema itazidi kuleta athari kwa wananchi. Askofu Mameo aliwataka viongozi wanaopewa dhamana kuwa na hofu ya Mungu katika utendaji wao wa kazi na kuweka maslahi ya taifa mbele ili kuleta maendeleo na kudumisha amani iliyopo.
 
Kwa upande wake, Mhashamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Telesphori Mkude, alisisitiza umuhimu wa waumini wa dini zote kuendelea kuliombea Taifa ili kuwa na amani hasa katika kipindi hiki cha mchakato wa kupata Katiba mpya.
 
Askofu Mkude aliwataka Watanzania kuepuka mifarakano na uvunjifu wa amani na badala yake wawe kitu kimoja hasa katika kipindi hiki cha kuibuka kwa rasilimali mbalimbali za taifa ikiwamo gesi na mafuta.

No comments:

Post a Comment