Kutemeba Katika Mapenzi na Kusudi la Mungu kwa ajili yako Kutakuletea tija Sana mwaka huu 2014.

Pastor Carlos Kirimbai Manna Tabernacle Bible Church

Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la BWANA ndilo litakalosimama. (MIT. 19:21 SUV).

Tafsiri ya Bibilia ya Habari Njema inasema:

Kichwani mwa mtu mna mipango mingi, lakini anachokusudia Mwenyezi-Mungu ndicho kitakachofanyika. (Methali 19:21 BHN).

Tafsiri ya Neno inasema:

Kuna mipango mingi ndani ya moyo wa mtu, lakini kusudi la BWANA ndilo litakalosimama.

Tukijumuisha yale yasemwayo katika tafsiri zote hizi tatu tunaweza kutoa muhtasari kwa kusema,

Japokuwa tunapanga mipango mingi ni ile iliyo sawa na kusudi la Bwana kwa ajili yetu ndiyo itakayo simama.

Sasa kama ni kusudi la Bwana ndilo litakalo simama, kwanini tupoteze muda kupanga mipango ambayo hatuna uhakika ni kusudi la Bwana au la kwa ajili yetu? Kwanini kusiwe na namna ya kujua kusudi la Mungu kwa ajili yetu ili tunapopanga mipango yetu tuipange kwa kuzingatia kusudi la Bwana kwa ajili yetu?

Tena maandiko yanaendelea kusema sehemu nyingine:

Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo. (EFE. 2:10 SUV).

Kumbe Mungu alipotuumba, alituumba ili tutende matendo mema fualni maalum ambayo yalishaandaliwa ili tuenende nayo. Sasa kwanini nisijue yale ambayo niliumbwa niyafanye alafu niyafanye?

Mungu anatuambia kwenye kitabu cha Yeremia:

Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. (YER. 29:11 SUV).

Kwa mujibu wa hili andiko yapo mawazo ambayo Mungu anatuwazia sisi. Ni mawazo ya mema na siyo ya mabaya, kutupa mwisho uliyojaa matumaini.

Tafsiri ya Bibilia ya Habari Njema inasema:

Maana, mimi Mwenyezi-Mungu ninajua mambo niliyowapangia. Nimewapangieni mema na si mabaya, ili mpate kuwa na tumaini la baadaye. (Yeremia 29:11 BHN).

Kwa hiyo ipo mipango ambayo. Mungu ametupangia. Ametupangia mema na si mabaya ili tuwe na tumaini la baadaye.

Sasa kama Mungu anayo mawazo mazuri kwa ajili yetu, na Mungu anayo mipango mizuri kwa ajili yetu, kwanini tusitafute kujua hayo mawazo na hiyo mipango ili nasi tuwaze na kupanga sawa na hiyo? Maana Yeye anajua kwanini alituumba na Yeye anajua alituumbia uwezo wa kufanya nini ndani yetu. Kwanini tusitafute kuyajua mawazo ya Mungu kwa ajili yetu na mipango hiyo aliyo nayo kwa ajili yetu ili tusiishi maisha yetu tukipoteza tu muda na mipango ambayo sio ya Mungu kwa ajili yetu ambayo haiwezi kufanikiwa hata hivyo?

Tafsiri ya Neno ya andiko hili la Yeremia inasema:

Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,’’ asema BWANA. “Ni mipango ya kuwafanikisha na wala si ya kuwadhuru, ni mipango ya kuwapa tumaini katika siku zijazo.

Mipango ya Mungu kwa ajili yetu itatufanikisha. Mafanikio yetu katika maisha haya yanategemea sisi kulifahamu kusudi la Mungu kwa ajili ya maisha yetu na kutembea katika hilo.

Napenda maneno ninayoyasoma katika kipande cha mstari kwenye kitabu cha Waefeso:

na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake. (EFE. 1:11 SUV).

Mungu hufanya mambo yote kwa kushauriana na mapenzi Yake kwa ajili yako. Kama hilo analotakwa alifanye litasaidia katika kudhibitisha mapenzi Yake katika maisha yako atalifanya. Kama analotakwa alifanye litavuruga mapenzi ya Mungu katika maisha yako, hakika hatalifanya.

Najuaje sasa mapenzi ya Mungu kwa ajili yangu? Naujuaje huo mpango wa Mungu kwa ajili yangu?

Kwanza kabisa badilisha kufikiri kwako. Anza kufikiri kwa namna ambayo kutaweka madai kwenye upeo wa kufikiri kwako juu ya kuujua mpango wa Mungu kwa ajili ya maisha yako.

Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. (RUM. 12:2 SUV).

Ukifanya upya nia yako utajua mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yaliyo kubalika na yaliyo kamili kwa ajili ya maisha yako.

Akili yako lazima igeuzwe. Akili yako lazima ibadilishwe. Kinachoweza kubadilisha akili yako kwa kiwango hicho ni kusoma kwako kwingi. Usomaji wako kwa wingi kutakugeuza akili yako na kupanga kufikiri kwa akili yako sawa na kusudi la Mungu na mapenzi ya Mungu kwa ajili yako.

Alipokuwa akijitetea hivi, Festo akasema kwa sauti kuu, Paulo, una wazimu, kusoma kwako kwingi kumekugeuza akili. (MDO 26:24 SUV).

Sasa ni nini hicho natakiwa kukisoma kwa wingi ili akili zangu zigeuzwe, zifanywe upya ili nipate kuyajua mapenzi ya Mungu kwa ajili yangu alafu nitembee katika hayo?

Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado. Mungu, fikira zako zina thamani nyingi kwangu; Jinsi ilivyo kubwa jumla yake! Kama ningezihesabu ni nyingi kuliko mchanga; Niamkapo nikali pamoja nawe. (ZAB. 139:16-18 SUV).

Siku zangu na zako zilizoamriwa na Mungu zimeandikwa chuoni mwa Mungu au katika neno la Mungu. Tunapokuwa wasomaji wazuri wa neno la Mungu, siku zetu zilizoamriwa na fikra au mawazo au mipango ya Mungu kwa ajili yetu inafunuliwa kwetu.

Kumbuka hili:

Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu. (ZAB. 119:105 SUV).

Neno la Mungu ni taa ya miguu yetu ikimaanisha itatusaida kuona tulipokanyaga, tulipo sasa hivi na ni mwanga wa njia yetu maana yake litatuonyesha tunapopaswa kwenda.

Nimalize kwa andiko hili:

Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, (Katika gombo la chuo nimeandikiwa,) Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (ZAB. 40:7, 8 SUV).

Ukishajua yale yaliyoandikwa kukuhusu kwenye gombo la chuo kwa ajili yako ni rahisi kuyafanya mapenzi ya Mungu uliyozaliwa kuyatumikia.

Jenga ukaribu na neno la Mungu. Lisome kwa wingi neno la Mungu. Litakufungua kuwaza ikupasavyo kwa habari ya mpango wa Mungu kwa ajili yako.

No comments:

Post a Comment