Ukombozi ambao Yesu alikuja Kutupatia (Tumewekwa huru mbali na Nguvu za Giza)

Mchungaji Carlos Kirimbai
I Yohana 3: 8b

8b Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.

Swali la kujiuliza hapa, je alidhihirishwa? Kama jibu ni ndiyo basi kazi za ibilisi zimevunjwa kama ni hapana basi hazijavunjwa na haziwezi kuvunjwa. Lakini jibu la swali ni ndiyo. Mwana wa Mungu amedhihirishwa kwa hiyo kazi za Ibilisi zimevunjwa sio zitavunjwa. Zimeshavunjwa na mpaka hili likuingie kwenye ufahamu wako itaonekana kama vile hazijavunjwa. Hupati shida kwa sababu hazijavunjwa unapata shida kwa sababu hii kweli hujaijua maana sharti ni kweli tu unayoijua ndiyo inayokuweka huru. Usipojua kuwa upo huru tayari utaendelea kusumbuliwa na vifungo japo kwa kweli upo huru.

Kuna maneno ya ajabu sana ambayo Paulo anawaandikia Wagalatia:

Wagalatia 4: 1 - 7.

1Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote; 2bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba. 3Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia. 4Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, 5kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana. 6Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba. 7Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.

Mimi na wewe kama watoto wa Mungu ni warithi sawasawa na ahadi za Mungu ila tukiendelea katika hali ya utoto hatutaonekana kuwa tofauti na watumwa japo ni bwana wa yote. Kazi ya mawakili na watunzaji ni kutufundisha kweli za neno la Mungu ambazo ndizo zinatufanya tukue katika ufahamu wetu wa Mungu na kile alichofanya kwa ajili yetu katika Kristo Yesu na kwa kadiri tunavyokua ndivyo tunavyozidi kuwekwa huru na kutembea katika ule uhuru ambao Kristo alitulipia pale msalabani.

Kutoka 23: 28 - 30.

28 Nami nitapeleka mavu mbele yako, watakaomfukuza Mhivi, na Mkanaani, na Mhiti, watoke mbele yako. 29 Sitawafukuza mbele yako katika mwaka mmoja; nchi isiwe ukiwa, na wanyama wa bara wakaongezeka kukusumbua. 30 Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako, hata utakapoongezeka wewe, na kuirithi hiyo nchi.

Tunaona katika mfano huu kuwa Mungu aliwaondoa maadui mbele zao kwa kadiri wao walivyokuwa wanaongezeka.

Kwa kadiri tunavyoongezeka katika kuijua na kuifahamu kweli kwa kadiri hiyo hiyo tutatembea katika uhuru uliyo haki yetu ya kiagano katika Kristo.

Paulo alipokuwa anazungumza na wazee wa Efeso alisema:

Matendo 20: 32.

32 Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa.

Haya maneno ya ajabu sana. Neno la Mungu linatujenga na kuachilia mikononi mwetu urithi wetu. Neno la Mungu linatupa kuifahamu kweli na hiyo kweli ndiyo inayotuweka huru.

Tukiangalia hili andiko hapa:

Wakolosai 1: 13:

13Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;

Alituokoa sio atatuokoa. Alituhamisha sio atatuhamisha. Imeshafanyika tayari ila mimi na wewe hatuwezi kutembea katika uhalisia wa kile kilichofanyika mpaka hii kweli tuikubali na tuielewe. Tusipoona kuwa hili jambo tayari limefanyika tutakuwa tunahangaika nalo kama jambo ambalo linatakiwa kufanyika wakati kwa kweli limeshafanyika na ukiokoka unaokolewa kutoka katika nguvu za giza na unahamishwa saa ile ile ambayo unaokoka. Sio kitu kinakuja kufanyika baadaye. Kinafanyika hapo hapo. Kunatokea badiliko la papo kwa hapo.

Tukiokoka kuna mambo matatu makuu yanatokea:

Wakolosai 2: 13 – 15.

13Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; 14akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; 15akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.

i). Tunasamehewa.

ii). Hati yetu ya mashataka inafutwa.

iii). Nguvu za giza kinyume na nasi zinavujwa.

Paulo aliuelezea wito wake hivi:

Matendo 26: 18.

18uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.

Swala la uhuru wetu ni swala la macho yetu ya ndani kufunguliwa tujue.

No comments:

Post a Comment