Viongozi wa dini wataka gesi inufaishe Watanzania

Viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali nchini wameitaka serikali kuhakikisha kwamba rasilimali ya gesi asilia inawanufaisha kwanza wazawa kabla ya kupelekwa nje.

Maombi hayo kwa serikali yalitolewa na viongozi hao wa dini mbele ya Rais Jakaya Kikwete katika kongamano lao lililofanyika jana jijini Dar es Salaam kujadili matumizi ya rasilimali za madini, gesi na mafuta kwa ajili ya manufaa ya Watanzania na taifa kwa ujumla.

“Pamoja na serikali kufungua milango kwa wawekezaji lakini iweke kipaumbele cha kwanza kwa wawekezaji wazalendo ili waweze kunufaika na rasilimali za nchi yao kisha iwatazame wawekezaji wa nje,” alisema Sheikh Abubakar Zubeir, aliyewasilisha maombi hayo kwa serikali kwa niaba ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata).

Sheikh Zubeir aliongeza: “Pamoja na kuwa makini na mikataba inayowekwa iwe ni kwa maslahi zaidi kwa nchi na wananchi wake na kuwalinda na athari mbaya zinazoweza kusababishwa na uwekezaji usiozingatia taratibu, sheria na kanuni na kuisababishia nchi kuingia kwenye matatizo.”

Viongozi hao waliongeza kuwa serikali haipaswi kusema kuwa Watanzania hawana mtaji wa kuvuna rasilimali hizo ikiwamo gesi asilia kwani kwa kufanya hivyo kunatoa mwanya kwa mataifa ya kigeni kunufaika nazo badala ya wazalendo.

“Kusema Watanzania hawana mtaji wa kuvuna rasilimali hizi ni sawa na kufumbwa macho, na ni mtazamo potofu kwani wageni wanatumia udhaifu huo huo kwa ajili ya kuja kutawala rasilimali zetu kwa kusema kwamba wao wenyewe wamesema, hatuwezi kuvuna gesi kwa kuwa hatuna mtaji,” alisema Dk. Padri Charles Kitima, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut).

Aliitaka serikali kuwapa wazawa uhuru wa kutafakari na kupendekeza maamuzi juu ya manufaa ya rasilimali za nchi na kwamba umiliki wa rasilimali hizo ndiyo unaofanya nchi husika kusonga mbele kiuchumi badala ya kusema inakusanya kodi huku wageni wakiendelea kunufaika nazo.

Padri Kitima pia aliwataka viongozi wa dini waliohudhuria kongamano hilo kuwafunda viongozi wa serikali ili wabadilike na kuwa waadilifu katika matumizi sahihi ya rasilimali hizo.

Pia, waliwataka Watanzania kutokubali kutumiwa kuhujumu rasilimali za nchi na kwamba wanapaswa kuwa na moyo wa uzalendo kwa kutambua kuwa rasilimali yoyote inapopatikana katika maeneo yanayowazunguka siyo yao pekee, bali kwa wananchi wote ili kulinda maslahi ya utaifa.

Kadhalika, waliitaka serikali kuweka taratibu nzuri za kulinda rasilimali za nchi ili ziwanufaishe wote sambamba kuundwa kwa taasisi zenye uadilifu.

Vile vile, viongozi wa dini waliitaka serikali kuwa makini na baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wanaotumia nafasi zao kuipotosha jamii na kuleta mafarakano na machafuko kwa ajili ya manufaa yao.

KAULI YA RAIS KIKWETE
Akizungumza kwenye kongamano hilo lililokusanya viongozi wa dini takribani 120 kutoka mikoa mbalimbali nchini, Rais Jakaya Kikwete alisema serikali itahakikisha sehemu kubwa ya gesi asilia itakakayovunwa inatosheleza kwanza mahitaji ya nchi kabla ya kuuzwa nje. Alisema haiwezekani gesi ikaanza kuuzwa nje ikiwa nchi bado haijanufaika vya kutosha kwa ajili ya maendeleo ya viwanda vikubwa.

Kuhusu ushiriki wa wazawa kwenye rasilimali za nchi, Rais Kikwete alifafanua kuwa, serikali haijaizuia kampuni yoyote, wala mtu au mbia yeyote kwenda katika ofisi za Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kununua fomu ya kuomba kutafuta rasilimali hiyo.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, kinacholeta malumbano makubwa kuhusu gesi ni kwa kampuni husika kutaka kupewa upendeleo na kutengewa eneo maalumu kwani utafutaji wa rasilimali hiyo hadi kuipata ni kama mchezo wa kubahatisha.

Aliongeza kuwa, rasilimali za nchi zisipolindwa vizuri zitaleta maangamizi badala ya neema kwani kuna nchi nyingi duniani ambazo zimeendelea kuteseka na matumizi mabaya ya utajiri wa rasilimali hizo.

Akitolea mfano wa mitambo ya kisasa iliyojengwa baharini kwa ajili ya kutafuta gesi, alisema utafutaji wake una gharama kubwa kwani unahitaji kampuni kubwa zenye fedha zake ambazo ni zaidi ya maelfu ya bajeti ya serikali ya Tanzania.

Rais Kikwete pia aliliagiza TPDC kujiandaa kuchukua leseni kwa ajili ya kuanza utafutaji wa gesi kama kampuni zingine zinazojitegemea badala ya kusimamia tu na kutangaza tenda.

Aliongeza kuwa kwa sasa serikali inataka kulifanya jiji lote la Dar es Salaam kuanza kutumia nishati ya gesi lengo ni kuokoa mazingira pamoja na kupunguza ukataji wa miti ovyo kwa ajili ya kupata mkaa wa kupikia.

Alisema serikali inatarajia kupata umiliki wa gesi wa asilimia 65 hadi 70 kutoka kampuni za ndani wakati kwa kampuni za nje itapata umiliki wa asilimia 70 huku asilimia 30 ikienda kwa kampuni husika.

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, alisema, rasilimali ya gesi ndiyo itakayowatoaWatanzania katika wimbi la umaskini kwani shughuli za uvuvi wa samaki na biashara ambayo ilianza enzi za utumwa, lakini hazijaweza kuwaondoa wananchi kutoka katika wimbi hilo.

Jumuiya za dini zilizowakilishwa ni Bakwata, Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Kanisa la Wasabato Tanzania (SDA).

Sorcce:Nipashe

No comments:

Post a Comment