Rais Kikwete afungua Kongamano la Viongozi wa Dini Kuhusu Matumizi ya rasilimali za Nchi, Gesi,Mafuta na Madini kwa Maendeleo ya Tanzania

Rais Kikwete akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Dini siku ya jana alipo kuwa akiwasili katika Kongamano hilo White Sand Jijini Dar es salaam,Kongamano hilo la Viongozi wa Dini Kuhusu Matumizi ya rasilimali za Nchi, Gesi,Mafuta na Madini kwa Maendeleo ya Tanzania
Rais Kikwete katikati walipopiga picha ya pamoja na viongozi wa Dini siku ya jana baada ya Kongamano hilo la Viongozi wa Dini Kuhusu Matumizi ya rasilimali za Nchi, Gesi,Mafuta na Madini kwa Maendeleo ya Tanzania. White Sand Jijini Dar es salaam


HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI UFUNGUZI WA
KONGAMANO LA VIONGOZI WA DINI KUHUSU MATUMIZI YA
RASILIMALI ZETU ZA GESI ASILIA, MAFUTA NA MADINI  KWA
AMANI NA MAENDELEO YA TANZANIA, WHITESANDS HOTEL,
TAREHE 20-22 JANUARI 2014

Waheshimiwa Viongozi wa Dini;
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa;
Ndugu Makatibu Wakuu;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;

Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema,
kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo kujadili matumizi
ya rasilimali zetu za gesi asilia, mafuta na madini kwa amani na maendeleo ya nchi
yetu.  Kwa  namna  ya pekee nawashukuru viongozi  wa  dini  kwa  kunishirikisha
kwenye  Kongamano  hili  muhimu  na  la  aina  yake.   Mmenipa  heshima  kubwa
ambayo sikuitegemea.  Asanteni sana.
Nawapongeza sana kwa uamuzi wenu wa busara wa kuandaa Kongamano
hili.   Mmedhihirisha kwa vitendo uhodari  wenu wa kutekeleza jukumu lenu la
msingi la kulea taifa letu kiroho na kushiriki kikamilifu katika masuala mengine
muhimu yahusuyo maendeleo na ustawi  wa Tanzania na watu wake.  Ninyi ni
wazalendo wa kweli.  Ni matumaini yangu na ya Serikali ninayoingoza kuwa ubia
wa aina hii utaimarishwa na kudumishwa kwa faida ya nchi yetu.
Najua mlianza kwa kukereketwa na athari  za matumizi  makubwa ya miti
kwa matumizi ya nishati jambo ambalo linachangia sana kuharibika kwa mazingira
duniani.  Mmeishia kwenye Kongamano hili.  Lina uwiano kabisa kwani tunakata
miti kwa ajili ya kuni na mkaa.  Tukitumia gesi itatoa huko.  Ni dhamira yetu hiyo.
Ndugu Viongozi wa Dini;
Kongamano  hili  linafanyika  katika  kipindi  mwafaka  kabisa,  kipindi
ambacho ugunduzi mkubwa wa gesi tayari umefanyika na dalili za kugunduliwa
zaidi zipo.  Kipindi ambacho hazina ya madini mbalimbali inazidi kugunduliwa na
makampuni ya utafiti yanatupa moyo kuwa mambo huenda yakawa mazuri zaidi.
Pia,  ni  kipindi  ambacho  rasilimali  zetu za  wanyamapori  na  misitu  zinatishiwa
kutoweka.  Ni kipindi ambacho wakulima na wafugaji na wafugaji na wahifadhi
wa misitu na wanyamapori wanashindania ardhi ya kufanyia shughuli zao. 

 Sasa
hivi ni kipindi mwafaka kabisa kukaa chini na kutafakari jinsi gani rasilimali hizi
zinaweza kulindwa na kutumika kwa manufaa ya nchi yetu na watu wake wote
zikiwanufaisha kule ambako rasilimali hizo zipo na hata kule ambako hazipo.    
Ni ukweli usiopingika kuwa Mwenyezi Mungu ameijalia nchi yenye utajiri
mkubwa wa rasilimali za asili.  Ametujaalia ardhi kubwa yenye rutuba, madini ya
aina mbalimbali,  misitu na mbuga za wanyama wa kila aina, hali ya hewa nzuri,
bahari, maziwa makubwa, mito mingi, watu wengi na kadhalika.  Rasilimali hizi,
kwa  tabia  yake,  inatakiwa  zitumiwe  vizuri  ili  kuboresha  hali  na  maisha  ya
Watanzania wote sawia na kwa miaka mingi na hata milele.  Vinginevyo rasilimali
hizi  zinaweza  kugeuka  kuwa  chanzo  cha  mifarakano,  magomvi  na  mauaji.
Zinaweza kuwa balaa na kuleta maangamizi  nchini  badala  ya kuwa baraka na
neema.
Mifano ipo ya nchi mbalimbali  duniani zilizojikuta zina migogoro na vita
vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na kugombania utajiri wao wa rasilimali za
asili.    Watu wa nchi hizo wanajuta kuwa na rasilimali ambazo zimekuwa chanzo
cha kuhatarisha amani,  utulivu, usalama na hata uhai wao.  Kwa hapa Tanzania
tunashukuru Mungu rasilimali hazijageuka kuwa balaa na tunaomba hilo lisitokee.
Tangu  Tanganyika  ipate  uhuru  na  Zanzibar  kufanya  Mapinduzi  Matukufu  na
hatimaye nchi zetu mbili kuungana  na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Serikali  za  awamu  zote  zimesimamia  kwa  makini  rasilimali  za  nchi  yetu  ili
ziwanufaishe Watanzania wote.  Tumetunga sheria na sera mbalimbali kuhakikisha
kuwa lengo letu hilo linatimia. 
Hata  hivyo,  usimamizi  wa sheria  hizo na utekelezaji  wa  sera  zetu nzuri
umekuwa  unakabiliwa  na  changamoto  mbalimbali  kwa  nyakati  mbalimbali.
Mpaka hapa tulipofika ni umahiri wa viongozi wetu ndiyo uliotuwezesha kuzuia
mambo yasiharibike na kugeuka kuwa matatizo makubwa.   Tumefanikiwa kiasi
chake ingawaje hatujaweza kuzuia kabisa matatizo yasitokee hapa na pale.  Taarifa
za kugombea rasilimali  zimekuwa zinasikika na nyingine zikiwa zimesababisha
watu kupoteza maisha, kujeruhiwa na mali kuharibiwa.  Tutafanya nini kukomesha
hali hiyo isijitokeze, ni jambo ambalo sisi kama taifa, yaani Serikali, wananchi na
wadau mbalimbali,  wakiwemo viongozi wa dini  hatuna, budi kulizungumza na
kulipatia ufumbuzi.


Ndugu Viongozi wa Dini;
Nimefarijika sana na uamuzi wenu wa kufanya mkutano huu kuzungumzia
rasilimali  ya mafuta na gesi.   Juhudi za kutafuta mafuta na gesi  imeanza tangu
ukoloni, zikaendelea katika awamu zote baada ya Uhuru. Shirika la Maendeleo ya
Petroli  (TPDC)  lilianzishwa  mwaka  1969 kuongoza juhudi  hizo na kusimamia
sekta ya mafuta nchini kwa manufaa ya Watanzania wote.  Hatujajaaliwa kupata
mafuta mpaka sasa lakini tumefanikiwa kupata gesi.  Ugunduzi wa kwanza wa gesi
asilia ulifanyika Songosongo mwaka 1971 na baadae Msimbati,  Mtwara mwaka
1982.  Utafutaji na ugunduzi huo uligharimiwa na Serikali yetu na hivyo gesi hiyo
ni mali ya Serikali.  Baada ya ugunduzi huo makampuni binafsi yalipata shauku ya
kutafuta mafuta na gesi nchini.
Mwaka 1980 ikatungwa Sheria ya Utafutaji wa Uzalishaji wa Mafuta kwa
nia ya kuweka masharti na utaratibu wa makampuni kushiriki katika utafutaji na
uzalishaji  wa mafuta na gesi  nchini.   Pia unatoa mwongozo wa mgawanyo wa
mapato  baina  ya  makampuni  na  Serikali.   Sheria  hiyo  imeendelea  kufanyiwa
maboresho  kwa  nyakati  mbalimbali  kulingana  na  mahitaji  ya  wakati  husika.
Kuanzia mwaka 2007 shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia ziliongezeka
kwa  nguvu  na  kasi  kubwa.   Juhudi  hizo  zilizaa  matunda  mwaka  2010  kwa
uvumbuzi  wa  kwanza  wa  gesi  katika  Bahari  Kuu uliofanywa  na  Kampuni  za
Orphir na British Gas.  Baada ya hapo ugunduzi umeendelea hadi kufikia futi za
ujazo trilioni 46.5 za rasilimali ya gesi nchini mpaka sasa.  Utafiti unaendelea na
matumaini ya kupata gesi  zaidi yapo.  Kufuatia ugunduzi huo, Tanzania sasa ni
moja ya nchi zimazohesabiwa kuwa na gesi nyingi duniani na ni nchi inayovutia
wawekezaji  wengi katika sekta ya gesi.   Kwa sababu hiyo, tukaamua kuifanyia
mapitio  Sheria  ya  Utafutaji  na  Uzalishaji  wa  Mafuta  na  Gesi.   Mwaka  2013
tumetunga  Sera  ya  Gesi  na  kurekebisha  masharti  ya  Mkataba  wa  Kugawana
Mapato yatokanayo na gesi  (Production Sharing Agreement)  na kuongeza mgao
wa Serikali.


Ndugu Viongozi wa Dini;
Sera  ya  Gesi  Asilia  iliyopitishwa  mwezi  Oktoba,  mwaka  jana  (2013)
imeeleza  wazi,  tena  kwa  lugha  nyepesi,  kuwa  gesi  ya  Tanzania  ni  mali  ya
Watanzania wote na itatumika kwa manufaa ya Watanzania wote – wa kizazi hiki
na kijacho.  Katika matumizi  ya gesi,  kipaumbele kitakuwa matumizi  ya ndani.
Msingi wa hoja yetu ni ule ukweli kwamba ukiuza nje gesi yote,  unapata mapato
peke yake lakini unakosa faida nyinginezo.  Ukiitumia ndani unapata mapato na
faida nyingine nyingi, kwa mfano, uzalishaji wa umeme, matumizi ya majumbani,
kwenye  magari  na  viwandani  kuzalisha  bidhaa  mbalimbali.  Hivyo  basi
mnapoitumia ndani gesi inakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya nchi yetu. 
Vilevile  tupo katika  mchakato  wa  kuandaa  sera  ya  kuwashirikisha  zaidi
Watanzania (Local Content Policy) ili wanufaike zaidi na rasilimali  yao ya gesi.
Kwa  sasa  nimewaagiza  TPDC  wajiandae  kushiriki  katika  utafutaji  wa  gesi,
uzalishaji  wake  mpaka  inapofika  sokoni.   Wasiwe  wagawaji  vitalu  tu  pekee.
Katika  sera  hiyo  mpya  pia  tunaangalia  shughuli  zinazoweza  kufanywa  na
Watanzania ili  tuone njia bora ya kuwawezesha kushiriki.   Kwa sasa tunadhani
wanaweza  kushiriki  kwa  urahisi  katika  utoaji  wa  huduma  kwa  kampuni
zinazofanya  utafiti  na  uzalishaji  wa  gesi  na  mafuta.   Wapo  walioanza  na
wanafaidika.  Nia yetu ni kuona idadi yao inaongezeka.


Mabibi na Mabwana;
Tumeanza  pia  mchakato  wa  kuiboresha  TPDC ishiriki  katika  uwekezaji
kwenye sekta ya mafuta na gesi kwa niaba ya Watanzania.    Katika utaratibu huo,
baadaye TPDC itauza hisa zake kwenye Soko la Mitaji ili Watanzania washiriki
moja ka moja katika kumiliki rasilimali hii muhimu.
Ndugu Viongozi wa Dini;
Mambo yote hayo yanafanyika ili kuhakikisha masilahi ya taifa yanalindwa
na  Watanzania  wote  wananufaika  na  rasilimali  zao  kwa  usawa.   Changamoto
kubwa tunayoiona kuhusu ushiriki wa Watanzania kwenye utafutaji na uzalishaji
wa mafuta na gesi  ni uwezo mdogo wa fedha, utaalamu na teknolojia tulionao.
Fedha zinazohitajika kwenye shughuli ya utafutaji mafuta na gesi, kwa mfano, ni
nyingi mno na Watanzania wenzetu hawanazo na hakuna uhakika wa benki iliyo
tayari kumkopesha mtu asiyekuwa nacho. 
Namna  nyingine  ni  kuwapa  maeneo  ili  wao  watafute  wabia  wawekeze.
Lakini,  mnapokuwa  mnasheria  inayoshirikisha  ubia  baina  ya  Serikali  na
mwekezaji,  kuamua kuacha Serikali  ili  badala yake apewe Mtanzania binafsi  si
uamuzi rahisi sana kuufanya.  Mtu binafsi ananufaika mwenyewe wakati Serikali
inanufaisha wengi.  Ninachokiona nafuu kufanya ni kutumia mwanya wa ushiriki
wa TPDC ili tuone baadhi ya hisa ziuzwe kwa Watanzania.  Hapa kunakuwa na
ubia wa TPDC na wananchi upande mmoja na Serikali upande mwingine.
Jambo  lingine  tunalolifanya  ni  kuhakikisha  kuwa  rasilimali  ya  gesi
inatumika vizuri, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazo vijavyo.  Tutaanzisha
mfuko maalum wa kuhifadhi mapato ya gesi na kuwekewa masharti ya matumizi
yake.  Tutatunga sheria maalum kwa ajili hiyo na tutafanya hivyo kwaka huu.


Mabibi na Mabwaba;
Kwa  upande wa  rasilimali  ya madini  mabadiliko makubwa  ya kiuchumi
yaliyoanza miaka 1980 katikati, Serikali ilijitoa katika uwekezaji na ikabaki kuwa
mhamasishaji  na  kuweka  mazingira  mazuri  ya  uwekezaji.   Kufuatia  hali  hiyo
wawekezaji wengi walianza kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali pamoja na
utafutaji na uchimbaji wa madini.  Serikali ikaweka Sera (1997) na Sheria (1998)
ya madini kusimamia sekta hiyo.  Ni kweli mapato ya Serikali na fedha za kigeni
ziliongezeka kutokana na uzalishaji wa madini.  Lakini palikuwa na manung’uniko
mengi kutoka kwa wananchi kuwa hawafaidiki sana na rasilimali zao.
Kamati  mbalimbali  ziliundwa  kuangalia  tatizo lipo wapi  ili  jawabu lake
litafutwe.   Nilipochaguliwa  kuwa  Rais  wa  nchi  yetu   mwaka  2005  niliyakuta
manung’uniko hayo na kuamua tuyatafutie jawabu.  Mwaka 2006 nikaunda Kamati
ya  Jaji  Bomani  ili  ichambuwe  mapungufu  yaliyopo na kutoa mapendekezo  ya
hatua za kuchukua.  Matokeo ya taarifa ya Kamati  ile ni Sera Mpya ya Madini
(2009) na Sheria Mpya ya Madini (2010).  Sera  na Sheria hii inalenga kuongeza
faida zaidi kwa Serikali na jamii, bila kuwasahau wale wanaozunguka migodi.
Faida  hizo  ni  pamoja  na  kuhimiza  kampuni  za  uchimbaji  wa  madini
kufungamanisha uchumi kati ya sekta ya madini na nyingine.  Vilevile tumewataka
waongeze nafasi ya ajira kwa Watanzania na ununuzi wa huduma na bidhaa nchini.
Aidha,  tumeamua  Serikali  iwe  inapata  hisa  katika  migodi  mikubwa
itakayoanzishwa siku za usoni.   Ndiyo maana tunaendelea kufanya mazungumzo
na kampuni  zitazochimba  uranium na  nickel.   Hatujamaliza  lakini  tunakwenda
vizuri.
Halikadhalika, Sheria na Sera vimeweka mkazo wa kuendeleza wachimbaji
wadogo  ambao  ni  Watanzania  tu.   Katika  kutekeleza  hilo,  tumeanza  kutenga
maeneo kwa ajili yao.  Changamoto kubwa inayowakabili  ni ukosefu wa mitaji,
vifaa na utaalamu.  Kuhusu fedha, tumeanzisha mfuko wa kuwasaidia na mwaka
huu wa fedha tumewatengea jumla ya shilingi bilioni 2.5.  Vile vile tunakamilisha
taratibu za kuanza kuwakodisha vifaa kupitia ofisi zetu za madini za Kanda.
Jambo lingine kubwa ambalo tunajiandaa kulifanya ili kunufaisha wananchi
na  nchi  yetu  ni  kutunga  Sheria  itakayohakikisha  kuwa  madini  mengi
yanayochimbwa  nchini  yanaongezewa  thamani  hapahapa  nchini.   Hatua  hii
itachangia sana kuongeza mapato na fursa ya ajira kwa watu wetu.


Nduvu Viongozi wa Dini;
Nimeyasema  haya  yote  kuwaonesha  kuwa  Serikali  haina  mchezo  katika
usimamizi wa rasilimali zetu za asili.  Tunafanya hayo kwa vile tunafahamu kuwa
zinaweza kutuletea maendeleo ya haraka.  Lakini pia zinaweza kusababisha nchi
yetu kuingia kwenye dimbwi la migogoro inayotokana na rasilimali.  Yote mawili
yanaweza kutokea kutegemea tutasimamiaje na kuzitumiaje rasilimali zetu.
Jambo  la  muhimu  ni  kusaidiana kuelimisha  jamii  ya  Watanzania  namna
tulivyojipanga  kusimamia  rasilimali  zetu  za  gesi  asilia,  mafuta  na  madini.
Waelewe  kuwa  utajiri  huu  ni  mali  yao  na  hivyo  ni  haki  yao  kunufaika  nao.
Wafahamu kuwa ni wajibu wao kulinda na kuzitunza rasilimali hizo ili zisipotee.
Ninyi mnayo dhamana ya kuelimisha jamii  waelewe nia hiyo njema ya Serikali.
Pia napenda kusema kuwa siyo kweli kwamba Serikali haijali rasilimali za nchi au
haitaki Watanzania wafaidike nazo; siyo kweli eti Serikali inapendelea wawekezaji
wageni kuliko wazawa na hakuna mkoa au eneo linapuuzwa au kubaguliwa.  Mimi
na  Serikali  ninayoiongoza  tutakua  watu  wa  mwisho  kupuuza  wazawa  na
kupendelea wageni au kupuuza watu wa maeneo ambako rasilimali  zinapatikana
au hazijapatikana.


Ndugu Viongozi wa Dini;
Naomba muendelee kutekeleza jukumu lenu la msingi la kulea taifa kiroho.
Mhimize waumini wenu wawe waadilifu na wazalendo.  Waache kujihusisha na
vitendo viovu vya wizi,  ubadhilifu,  matumizi  mabaya ya madaraka na rushwa.
Mkifanikiwa hilo, rasilimali zetu zitakuwa salama.  Vile vile muendelee kuhubiri
upendo miongoni mwenu, miongoni mwa waumini wenu na miongoni mwa watu
wote.  Watu wakumbushwe kuwa sisi wote ni viumbe wa Mungu na mbele yake
sisi  wote  ni  ndugu na  inabidi  kuheshimiana  na  kuvumiliana  kwa  tofauti  zetu.
Tukifaulu kwenye hili nchi yetu itabaki salama daima milele.
Nafahamu  kuwa  wapo  baadhi  ya  watu  ambao  wanafanya  vitendo  vya
kuhujumu rasilimali  zetu.  Wapo wanaoingia mikataba isiyozingatia maslahi ya
taifa  katika  uvunaji  wa  rasilimali  zetu.   Wapo wengine  wanaokula  njama  na
wawekezaji  ili  Serikali  ipunjwe mapato yake.  Watu wa aina hiyo wapo katika
jamii  ye yote ile na sisi  kuwa nao si ajabu.    Napenda mfahamu kuwa Serikali
inapinga vitendo vya aina yoyote vya kuhujumu rasilimali  zetu.  Ndiyo maana
watu  wa  aina  hiyo  wanapobainika,  wanachukuliwa  hatua  na  vyombo
vinavyohusika.  Ninyi pia msichoke kuwafichua, wapo miongoni mwa waumini
wenu.


Mabibi na Mabwana;
Kabla  ya  kumaliza,  napenda  kumshukuru Waziri  wa  Nishati  na  Madini,
Profesa Sospiter Muhongo na timu yake Wizarani kwa kushirikiana na viongozi
wa dini katika jambo hili  muhimu.   Naamini hatua hii  ya kuwapa taarifa sahihi
viongozi  wa  dini  kuhusu  matumizi  ya  rasilimali  zetu  hususan  gesi  na  madini
itasaidia  kuongeza  uelewa  wa  waumini  wenu  na  wananchi  kwa  jumla.
Watafahamu fursa zilizopo na jinsi ya kuzitumia ili wafaidike nazo.  Nakushukuru
pia kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa sera na mipango ya Serikali katika sekta
ya nishati na madini.  Kazi yenu nzuri inaonekana na sisi wote ni mashahidi.
Mwisho,  nawashukuru  viongozi  wa  dini  kwa  kunishirikisha  kwenye
Kongamano lenu.  Naamini mkitoka hapa mtakuwa mabalozi wazuri wa kueneza
ujumbe kuwa rasilimali za Watanzania zipo kwenye mikono salama. Baada  ya
kusema hayo, napenda kutamka kuwa Kongamano la Viongozi wa Dini kujadili
matumizi  ya  rasilimali  zetu  za  gesi  asilia,  mafuta  na  madini  kwa  amani  na
maendeleo ya nchi yetu limefunguliwa rasmi.  Nawatakia kila la heri na mafanikio
katika mwaka huu wa 2014. 
Asanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment