Viongozi wa dini watembelea bomba la gesi asilia Mtwara

Mtambo wa usafishaji gesi asili uliopo eneo la Mnazi bay Mkoani Mtwara
Viongozi wa Dini wamesema lengo la Wizara ya Nishati na Madini kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wa dini katika sekta za gesi na mafuta kwa manufaa ya Watanzania limefikiwa.

Akizungumza baada ya ziara ya kutembelea bomba jipya la gesi asilia Mtwara- Dar es Salaam, mtambo wa kusafisha umeme wa Mnazi Bay na maeneo mbalimbali ya uendelezaji wa gesi asilia katika mikoa ya Mtwara na Lindi, Katibu wa Jumuiya ya Kikrsito Tanzania (CCT) na Mwenyekiti wa Sekretariati ya kongamano la viongozi wa dini, John Mapesa, alisema viongozi wa dini wamepata elimu sahihi ambayo hawakuifahamu kabla kuhusu sekta hizo.

Alisema viongozi hao wamekuwa wakipata habari ambazo si sahihi kuhusu rasilimali hizo, lakini baada ya kutembelea, kujifunza, kuona na kusikia kutoka kwa watalaam mbalimbali kuhusu namna miradi hiyo inavyofanyika, wanatarajia kuwa walimu kwa Watanzania wengine ili kuwa na uelewa wa pamoja.

Aliongeza kuwa viongozi wa dini ni sehemu ya jamii na wanaposhirikishwa kwa kuelezwa mipango mbalimbali ya serikali, ni jambo la muhimu kwa sababu wanayo nafasi ya moja kwa moja ya kuwasiliana na wananchi ikiwamo kushauri.

Aliongeza kuwa elimu waliyoipata na taarifa walizozipata, zitakuwa na mchango katika kuleta amani na ustawi wa jamii wakati huu ambapo nchi inaelekea katika kupokea uchumi mkubwa kupitia rasilimali hizo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini aliyeongoza ujumbe huo, Ngosi Mwihava, alisema kufuatia ziara hiyo ya viongozi wa dini, inaonyesha kuwa serikali ni inasikiliza matarajio ya wananchi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Abdallah Ulega, aliutaka ujumbe huo kuwaeleza wananchi kuwa mafanikio katika sekta ya gesi yapo na wananchi wameanza kufaidika nayo.

Chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment