Askofu Paschal Kikoti afariki dunia



Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda, limepata pigo la kumpoteza askofu wake wa kwanza, Paschal William Kikoti (55), aliyefariki dunia kutokana na ugonjwa wa shinikizo la damu katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza.

Taarifa za kifo kicho zilitolewa kwa waumini juzi usiku katika Kanisa Kuu la kiaskofu na Makamu Askofu wa jimbo hilo, Padre Patrick Kasomo.

Alisema kuwa Askofu Kikoti alipatwa na ugonjwa wa shinikizo la damu Jumapili iliyopita, majira ya saa moja asubuhi wakati akioga bafuni, na ndipo alipoanguka ghafla kisha kupoteza fahamu.

Padre Kasomo alifafanua kuwa, Askofu Kikoti aligunguliwa baadaye na mapadri na masista walipokuwa wametoka kwenye ibada ya misa ya kwanza saa 2:30 asubuhi huku akiwa ajitambui.

“Baraza la Maaskofu lilitafuta usafiri wa ndege siku hiyo, ambayo ilimsafirisha hadi mkoani Mwanza na kupelekwa moja kwa moja katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya matibabu hadi hapo juzi saa 2:30 jioni alipofariki dunia,” alisema.

Taarifa hiyo ya Padre Kasomo, iliwashtua waumini wengi ambapo baadhi yao walishindwa kujizuia na kujikuta wakiangua vilio na wengine kuzirai.

Askofu Kikoti alizaliwa mkoani Iringa katika Parokia ya Nyabula mwaka 1957 na kupewa daraja la upadre Juni 29, 1988 humo humo mkoani Iringa.

Mnamo Januari 14, 2001 Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, aliliunda jimbo jipya la Mpanda na kumteua Kikoti kuwa askofu wa kwanza kuliongoza.

Kuhusu mazishi, Padre Kasomo alisema kuwa mwili wa marehemu Askofu Kikoti utawasili jimboni humo kwa ndege leo ukitokea Mwanza na unatarajiwa kuzikwa rasmi Jumamosi katika Kanisa Kuu la Kiaskofu Mpanda.

No comments:

Post a Comment