Kituo cha Sheria watoa elimu ya Katiba Kanisani

Kituo  cha Sheria na Haki za Binadamu, kimetoa elimu ya katiba katika kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Ubungo Christian Centre la jijini Dar es Salaam ili waumini waweze katika mchakato wa kutoa maoni yao katika mchakato wa marekebisho ya uundwaji wa katiba mpya.

Elimu hiyo ilitolewa na wanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kwa muda wa siku mbili kanisani hapo, ambapo walibainisha kuwa, wakristo wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali ambazo wanaweza kutoa maoni na wakaweza kupata kile wanachokitaka pasipo kuvunja sheria.

Logo ya Kituo  cha Sheria na Haki za Binadamu

Anna Henga, mmoja wa wanasheria wa Kituo hicho cha Sheria na Haki za Binadamu chenye makao makuu yake Kijitonyana jijini Dar es Salaam, alisema Ibara ya 19 inayozungumzia uhuru wa kuabudu, alieleza kwamba wakristo wanapaswa kutoa maoni yao ili kuondoa dukuduku na ukiritimba unaohusu vibali vya kuhubiri Injili, ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa na wachungaji kwamba vinawanyima uhuru.

Akitilia msisitizo juu ya hilo alichanganua kwamba, Katiba iliyopo ambayo ni ya tano ina viraka vingi ambavyo kwa sasa vina mapungufu yanayohitaji maoni ya watu wa Mungu ili kuandikwa katiba mpya; alivitaja vichache, kwamba ni pamoja na masuala ya dini kutoingiliwa na serikali kabisa kwa kuwa uhuru wa kuabudu unapaswa kuwekwa katika haki za binadamu; ukiheshimiwa na usiotakiwa kuguswa .

Mbali na hilo alieleza kwamba, wakristo wengi wanafikiri kuomba tu na kukaa kimya ndiyo jibu la matatizo yao, huku akibainisha kwamba hata mtume Paulo alipopelekwa kwa Pilato ingawa aliomba lakini ilipofika wakati wa kujitetea alisema na yeye ni Mrumi wa kuzaliwa na hilo lilimfanya kuachiwa huru.

Kama hilo halitoshi alibainisha kwamba, wakristo wengi wamekuwa na kigugumizi juu ya kuwepo kwa mahakama ya Kadhi nchini, ambapo alieleza kwamba kwa maoni yao kunaweza kuleta mahakama moja kwa watu wote, kwa haki zote hupatikana mahakamani na katiba ndiyo sheria mama.

“Ikiwa mtanyamaza basi mtaiona ikianza kufanya kazi,’ alisema Bi. Anna.

Kuhusu mfumo wa Serikali; alieleza kwamba, yapo mambo ambayo yanalalamikiwa mara kwa mara na wananchi ambayo ni kuhusu Tume ya uchaguzi, ambapo alisema inabidi kuwepo kwa tume huru; isiyoundwa na chama kimoja wakati huu wa vyama vingi. 

Mwonekano wa Katiba ya Tanzania kwa juu.
Akitaja baadhi ya udhaifu uliopo ndani ya katiba iliyopo alisema kuwa ni; madaraka makubwa aliyo nayo rais, haki za binadamu kuwekwa wazi kuhusu Afya, elimu na walemavu, Jaji Mkuu asiwe wa chama kimoja, hukumu ya kifo iliyopo si haki kuondoa uhai wa mwingine, vyombo nyeti kama Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali na Spika wa bunge asitoke katika chama fulani.

Aliendelea kueleza kwamba udhaifu mwingine ni; Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, tume ya maadili ya viongozi, pia mihimili mikuu mitatu: Mahakama,  Bunge na serikali iwe huru, isiingiliwe au kupata shinikizo kutoka upande wowote.

Pia aliongeza kwa kushauri kuwa ni vyema Muungano wa Tanzania na Zanzibar uangaliwe upya, pia Tume ya Uchaguzi kuwa huru.

“Tanzania ni nchi isiyoongozwa na dini inayofuata mfumo wa kisekula, haifungamani na dini yoyote jambo ambalo limeifanya nchi kuwa shwari bila kuwa na vita vya kiudini; hivyo katiba isiingize masuala ya imani ya mtu au watu,” alisema.

Akiwashukuru waalimu hao; Mchungaji Paulo Mulokozi wa TAG Ubungo Christian Centre (UCC) alihimiza Wakristo kushiriki kutoa maoni yao katika mchakato wa kupata katiba mpya ya taifa na pia kushiriki vyema katika sensa inayotarajiwa.

“Tumekuwa tukiliombea taifa letu kila mara, lakini hiyo haitoshi lazima tushiriki kikamilifu kutoa maoni yetu katika mchakato wa kuunda Katiba mpya, kushiriki sensa na kuchukua fomu za uongozi inapobidi,” alisema Mchungaji Mulokozi, na kuongeza: “Tutakuwa hatutendi vyema kama watu wa Mungu tusiposhiriki kikamilifu kama watanzania.”
  
Mchungaji aliwapongeza na kuwashukuru wawezeshaji hao kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu; Bi. Flaviana Charles na Anna Henga, na kusisitiza Wakristo wengi kujitokeza ipasavyo katika kutoa maoni, na hata katika kupiga kura; pia kushiriki kwenye kura na sensa.


No comments:

Post a Comment