Kanisa la TAG kufanya Uchaguzi wa Askofu Mkuu Dodoma

Askofu Mkuu Dk. Barnabas Mtokambali

MKUTANO Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), ambao unafanyika kila baada ya miaka minne unaoambatana na uchaguzi wa viongozi wa ngazi mbali mbali, unaanza  Jumatano tarehe 8, Agosti mjini Dodoma na kuendelea kwa karibu wiki nzima.

Kwa mujibu wa takwimu za makao makuu, zaidi ya watumishi wa Mungu 3000 wanatarajia kukutana Dodoma  na Mkutano Mkuu utafanyika katika Chuo Kikuu cha  Dodoma, ukitanguliwa na  vikao vya Halmashauri kuu  na Baraza la Waangalizi.

Akiongea na waandishi wa habari, katika mahojiano maaalumu wiki iliyopita,  Naibu Katibu Mkuu (Shughuli) wa kanisa hilo, Mchungaji Uswege Mwakisyala, alisema kuwa, mkutano huo mkuu utafanyika Chimwaga mjini Dodoma, na watu watakaohudhuria wanakadiriwa kufikia  3000,  ingawa sio wote watakao piga kura.

Mchungaji Mwakisyala alieleza kuwa, siku ya Jumatatu (Agosti 6, 2012) kutakuwa na kikao cha Halmashauri Kuu, huku kikifuatiwa na kikao cha Baraza la Waangalizi kitakachofanyika siku ya Jumanne.

Alibainisha kwamba siku ya Jumatano ndio mkutano mkuu utaanza kufanyika ambao utahitimishwa Ijumaa.

Hata hivyo Mchunagji Mwakisyala akitolea ufafanuzi juu ya utaratibu wa kuwasili mkoani humo alitanabaisha kwamba, Halmashauri Kuu watawasili siku ya Jumapili, tayari kwa kuanza kikao Jumatatu na waangalizi watawasili Jumatatu.

Mbali na hilo aliongeza kwamba, Wachungaji wote watakaowasili siku ya Jumanne, Agosti 7, 2012 watatakiwa kwenda moja kwa moja katika chuo kikuu cha Dodoma (UDOM).

“Jumapili watawasili Halmashauri Kuu, Jumatatu Baraza la Waangalizi na Jumanne wachungaji wote, na itakuwa ni vizuri ikiwa wataingia kwa makundi makundi, kwa kufanya hivyo magari yatawaingiza moja kwa moja hadi  chuoni,” alisema.

Katika mkutano huo mkuu, Kwaya mbalimbali na waimbaji binafsi watasindikiza uchaguzi huo.

Uchaguzi uliopita ulifanyika Oktoba 2008, ambapo Askofu Mkuu Dk. Barnabas Mtokambali, alichaguliwa kuliongoza kanisa hilo, huku Makamu wake akiwa Dk. Magnus Muhiche, na nafasi ya Katibu Mkuu ikichukuliwa na Mchungaji Ron Swai.

Katika muhula wao wa uongozi, Askofu Mkuu, Dk. Mtokambali, na timu yake walikuja na Kauli mbiu ya Miaka Kumi ya Mavuno iliyokuwa na lengo la kuleta watu milioni mbili kwa Yesu.

Wakati wanaingia madarakani, kanisa hilo lililokuwa na waumini 200,000 mwaka 2008, lakini hadi sasa (Mwaka 2012) lina waumini 433,546. Wachungaji walikuwa 2600 sasa wako 4527, makanisa yalikuwa 2134 sasa yako 4492.

Pia Seksheni zilikuwa 75, lakini sasa ni 204 huku majimbo nayo yakibadilika kutoka 10 hadi 25.

Kimsingi uchaguzi wa TAG, huongozwa na Roho Mtakatifu mwenye na hakuna wagombea wala kampeni, bali Bwana mwenyewe hujitwalia viongozi.
Wasimamizi wa uchaguzi wanatarajiwa kuwa wamisheni kutoka Marekani.

No comments:

Post a Comment