Pallangyo Brothers wampa shetani kipigo Uyole Kati

Waimbaji watatu kutoka Arusha, wanaounda kundi la Pallangyo Brothers, wenye kimo kifupi (Kibirikizi) kwa kushirikiana na Kanisa la flani Uyole Kati mjini Mbeya, wameleta mamia msalabani katika mkutano mkubwa wa Injili wa siku sita.

Mkutano huo uliokuwa ukiendeshwa katika viwanja vya Kanisa hilo, huku Mhubiri akiwa Askofu Steven Mulenga toka Mombo mkoani Tanga, uliokusanya mamia ya wakazi wa mji huo, waliokuwa wakisumbuliwa na mapepo, huku wengine wakibubujikwa na machozi baada ya kutua mizigo yao msalabani.

Akihubiri katika mkutano huo, Askofu Mulenga, huku akisindikizwa na ujumbe uliokuwa na kichwa kisemacho; FILIPO ALIVYOMDHIBITI  SIMONI MCHAWI KWA JINA LA YESU, alisema, Yesu alidhihirishwa ili kuzivunja kazi zote za shetani.

Alibainisha kwamba, mwanadamu yoyote akimwamini Mungu ni wazi kuwa hakuna jambo lolote linaloweza kushindikana, huku akielezea kwamba, dhambi ndiyo inayomtenganisha mwanadamu na Muumba wake.

Mtumishi huyo aliweka wazi juu ya hilo alisema: “Hata leo Yesu yu hai na anaweza kumpa mtu mahitaji yake wakati wowote anapoitwa.”

Askofu Malenga, huku akiwa sambamba na Mchungaji mwenyeji wa Uyole Kati, Immanuel Mwalyenga alitanabaisha kwamba, hata yale ambayo watu wameyakatia tamaa, Bwana anaweza kuleta ukombozi na kumuaibisha shetani.
Katika mkutano huo, Pallangyo Brothers walikuwa na mguso wa pekee kwa jamii, huku watu wakijiuliza namna maumbo yao yalivyo, lakini wanaweza kumnyang’anya shetani mateka.
Huduma ya uimbaji katika mkutano huo, mbali na kuwepo kwa Pallangyo Brothers pia walikuwepo wengine kama akina Amani Mwasote, Kwaya kutoka makanisa mbalimbali na kwaya wenyeji Usiogope na Kedroni.
Ingawa mkutano huo ulifanyika wakati wa kipindi cha maonesho ya Kikanda ya Nanenane ambayo pia huvuta watu wengi, lakini Mungu hakuweza kuruhusu shetani afanye uharibifu kwa kuwakalia watu wa Mungu na hivyo kwa uwingi wao walikusanyika kwenye mkutano huo mkubwa.
 Katika mkutano huo watu zaidi ya 60 waliokolewa, wengine walifunguliwa katika vifungo vya magonjwa na maonezi ya pepo wabaya, huku wengine wakileta vitu vyao ambavyo walitumia kwa uganga vichomwe moto.
Moja ya vitu vilivyomuacha shetani taabani ni la mama mmoja kutoka kijiji cha Isyonje wilayani Rungwe ambaye baada ya kusikia tangazo la mkutano kupitia Redio Ushindi, alisafiri hadi Uyole kusikia Bwana anasema nini juu ya maisha yake na katika siku ya pili ya mkutano alifunguliwa kutokana na mapepo ambayo yalikuwa yamemtesa kwa muda mrefu.
Kama hilo halitoshi, mwisho wa mkutano Askofu Mulenga wakishirikiana na Mchungaji Kiongozi wa Uyole Kati Immanuel Lyego Mwalyenga, pamoja na jopo la wachungaji waliohudhuria mkutano huo, walifanya maombi ya kuliombea Taifa kwa kushika bendera ya Tanzania.
Waamini hao wapya, waliompokea Bwana Yesu katika mkutano huo; wanaendelea na mafundisho ya msingi yanayoongozwa na Mchungaji Bahati Mwandemba katika kuhakikisha wanaendelea katika imani na kufanyika baraka kwa Kanisa, Taifa na jamii kwa ujumla

No comments:

Post a Comment