RC, Paroko kutokomeza mauaji kanda ya ziwa

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Evarist Ndikilo.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo kwa kushirikiana na Paroko Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Nansio, Padri Charles Masaga wameahidi kutokomeza mauaji ya kishirikina yanayofanywa na kikundi cha Makilikili na kusababisha hofu kwa wakazi wa Ukerewe.

Rai hiyo ilikuja baada ya Mkuu wa Mkoa  wa Mwanza  kuelezwa kwa nyakati tofauti na wakazi,  wilayani humo kuwa kundi hilo linajihusisha na mauaji ya watu na kisha kunyofoa viungo vya mwili hasa sehemu za siri.

Akiwa katika kijiji cha Bugorola Ndikilo alielezwa kuwa, hivi sasa wakazi wa Wilaya hiyo wanashindwa kutimiza majukumu yao vyema wakihofia kuuawa na kundi ambalo hata hivyo wahusika wake hawajulikani.

Mkuu huyo wa Mkoa ambaye alikuwa katika ziara ya siku mbili wilayani Ukerewe kuhamasisha  sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agositi 26, 2012 aliahidi kuwa serikali ikitumia vyombo vyake vya dola itafanya kila linalowezekana kuhakikisha  vitendo hivyo vinakomeshwa.

Alisema vitendo hivyo vimekuwa vikilalamikiwa na watu wengi na kwamba wanajipanga kuhakikisha wanalimaliza kabisa kwa sababu liko chini ya uwezo wao.

Naye Paroko wa Parokia ya Nansio, Padri Masaga akiongelea jambo hilo, huku akiahidi kuwa bega kwa bega na kamanda huyo; aliitaka serikali kutokaa kimya badala yake ikemee maovu hayo, ikiwa ni pamoja na vitendo vya ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu serikalini.

Mtumishi huyo wa Kanisa Katoliki ambaye aliendelea kubainisha kwamba anasikitishwa na tabia ya serikali kubaki  kimya bila kutoa tamko na hata kukemea mambo kama haya ya mauaji ya watu na kisha kunyofolewa viungo sehemu za siri na  kikundi cha Makilikili.

Hata  hivyo uchunguzi wa Polisi unaonyesha kuwa  hofu hiyo imesababishwa na uvumi ulioenea  takribani miezi miwili iliyopita, baada ya kuwepo vifo vya watu watatu ambao kati yao wanaume wawili wamepigwa hadi kufa kwa tuhuma za wizi; huku mwanamke mmoja akipoteza maisha katika harakati za kutoa mimba.

Wakati huo huo; watu watatu wamekufa maji wilayani Ukerewe, Mwanza baada ya mtumbwi wao kupigwa na dhoruba na kuzama katika ziwa Victoria.

Habari zilizopatikana  toka kisiwa kidogo cha Kweru na kuthibitishwa na Polisi zinasema kuwa katika mtumbwi huo wa kasia walikuwemo watu 15  na kati yao watatu walikufa  maji huku wengine 12 wakiokolewa na wavuvi waliokuwa karibu na eneo hilo.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Mery Tesha alisema watu hao walikumbwa na mkasa huo wiki iliyopita majira ya saa 10.00 jioni, wakati wakitokea kijijini kwao Buzegwe kwenda kisiwani Kweru kuhani msiba wa ndugu yao.

Habari zaidi zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Leberatus  Barlow zimewataja waliokufa kuwa ni  Mgalla Yustinian (55), Pascazia Lyaganga (55) wakazi wa kijiji cha Buzegwe na Nyanjala Dotha (45) ambaye ni mkazi wa  kijiji cha Bukongo.

Diwani wa kata ya Kagunguri, Misana Ghatawa, akiongelea tukio hilo, alisema watu hao walipata mkasa huo muda mfupi baada ya kuondoka katika mwaloni wa Ilondo, miili yao tayari imepatikana na kuchukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi.

Baadhi ya wavuvi walioshuhudia tukio hilo walisema, mtumbwi huo ambao ulionekana kulemewa na mzigo, ulizama baada ya kupigwa na mawimbi makubwa ya ziwa Victoria na kuongeza kuwa, kama wangekuwa na vifaa vya uokozi pengine wote wasingepoteza maisha.

No comments:

Post a Comment