Askofu Mokiwa atangaza masamaha kwa waliopinga uteuzi wa Askofu

Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana nchini, Dk Valentino Mokiwa
Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana nchini, Dk Valentino Mokiwa ametangaza msamaha kwa waumini waliofungua kesi kumpinga Askofu Stanley Hotay kusimikwa.

Asofu Mokiwa ametangaza msamaha huo wakati Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo akiwaomba viongozi wa dini kiliombea taifa liepukane na wenye tamaa ya urais.

Askofu Dk Mokiwa na Mulongo walitoa kauli hizo kwa nyakati tofauti wakati wa ibada maalumu ya kusimikwa kitini kwa Askofu Hotay kwenye Kanisa la Christ Church Jijini Arusha.

“Waliofikiria kwamba Kanisa litatumia nguvu ya kutenga dhidi ya waliosababishia Kanisa aibu iliyotukumba watakakuwa wamekosea. Kanisa linatumia kauli ya Yesu Kristo kuwaombea msamaha kwa Mungu kwani hawajui walitendalo,” alisema Askofu Dk Mokiwa.

Hata hivyo aliwaasa waumini watatu waliofungua kesi mahakama kuu kumpinga Askofu Hotay na wote waliowaunga mkono katika uamuzi huo kurejesha imani yao kwa Mwenyezi Mungu na kudumu katika hofu ya Kristo badala ya kufikiria kutenda dhambi nyingine ya kupinga kazi ya Mungu.

Akitoa salamu za Serikali katika ibada hiyo, Mkuu wa Mkoa alielezea kusikitishwa na tabia iliyoibuka miongoni mwa Watanzania kwa kila mmoja kutaka kuwa Rais kwa kumvunjavunja na kumkwamisha Rais
aliyeko madarakani.


“Zamani watu walioandaliwa na kuchujwa kuwa viongozi kwenye madhehebu ya dini kama wachungaji na maaskofu. Hata marais waliandaliwa. Lakini siku hizi mtu anakaa nyumbani kwake, anajipima na kujisemea kuwa
ametosha urais na kuunda kukindi cha kumsemea na kumpigania,” alisema Mulongo.

Huku akishangiliwa kwa nguvu na waumini, Mulongo alisema tabia hiyo huchochewa na uroho wa madaraka na kuwataka wanaotamani uongozi kusubiri walioko madarakani wamalize kipindi chao.

Aliwapa changamoto viongozi wa dini kuliombea taifa na kukemea kwa uwazi na ukweli maovu yote yanayotokea ndani ya jamii ikiwemo watu kutopenda kutii sheria na ufisadi, matendo aliyosema yanatendwa na waumini wao makanisani na misikitini.

Kwa upande wake Askofi Hotay naye aliungana na kauli ya Askofu Mkuu Dk Mokiwa kwa kutangaza msamaha kwa wote waliompinga na kuwaomba waanze maisha mapya kwa kutumia akili kwa lengo la kutangaza utukufu na
ufalme wa Mungu badala ya kulumbana kwa utumishi wa kiroho.

Ibada hiyo ilihudhuriwa na maaskofu Saba kutoka Dayosisi mbalimbali za Kanisa Anglikana ndani na nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment