CASFETA kuleta ukombozi kwa vijana.

 Wadhamiria kuikabili Zanzibar kiinjili        
Moja ya mikakati ya Umoja wa wanafunzi Wakristo waliookoka “The Christian Ambassadors Student Fellowship Tanzania,” ni kuhakikisha kuwa wanamkomboa kijana wa kitanzania kutoka utumwani wa ibilisi na kuishi maisha ya kumpendeza Kristo, akiacha kutumikishwa na shetani.

 Hayo yalisemwa hivi karibuni na Rais wa CASFETA Tanzania, Kelvin Ngonyani,  katika mahojiano maalumu na Blog, katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG),  City Christian Centre (CCC), lililopo Upanga jijini Dar es Salaam,  kwenye ibada maalumu ya kusifu na kuabudu.


Rais huyo aliongeza kuwa mipango mikubwa waliyo nayo ni kumhubiri Kristo katika hali yoyote, huku akibainisha kuwa, moja ya mikakati waliyonayo ni kuimarisha huduma hiyo katika Visiwa vya Zanzibar kwa lengo la kuwakomboa vijana na watanzania visiwani humo kuacha kumtumikia ibilisi.

“Tuna mikakati mingi sana, lakini mkubwa zaidi ni kuhubiri injili katika kila eneo la nchi hii, lengo ni kumkomboa kijana na mtanzania kuacha kutumikishwa  na shetani, pia  tutahakikisha tunaibadili Tanzania,  kwa upande wa Zanzibar tumeisha anzisha Casfeta,  lakini tunataka tuiboreshe zaidi,  tunamwamini Mungu tutafanikiwa,” alisema Rais huyo.

Mbali na hilo aliweka wazi kwamba mbali na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo, bado wamekuwa wakimuona Mungu akiwa upande wao na akiwafanikisha kwa kiwango kisicho cha kawaida, huku akiongeza kuwa moja ya mafanikio hayo ni kuongezeka kwa wana CASFETA kutokana na makongamano kadhaa ambayo wamekuwa wakiyafanya mashuleni ambapo  hutumia fursa hiyo kuihubiri injili na vijana wengi kumrudia Kristo.



Chanzo cha Blog kilipata fursa ya kuzungumza na Mchungaji msaidizi wa Kanisa la City Christian Centre Upanga, Deus Cheyo, aliye hudhuria ibada hiyo, ambapo alisema kuwa vijana wengi wamekuwa wakipotea kutokana na kukua kwa Teknolojia, hivyo kujifunza mambo yasiyofaa, na kupelekea maadili kushuka.
Katika hilo, Mtumishi huyo wa Mungu akawataka wazazi kuwapa elimu na mafunzo ya msingi wa Biblia watoto wao jinsi dunia ilivyo kwa sasa, ili kukinusuru kizazi hiki ambacho shetani anakitafuta kwa kasi ya ajabu akiangamize.

 Aliwataka  watumishi wa Mungu kuwa na ibada za vijana makanisani kwa lengo la kufundishwa Neno na jinsi ya kukabiliana na changamoto za dunia.

Mchungaji huyo ambaye pia alipata nafasi ya kutoa Neno katika ibada hiyo, aliwataka mamia ya wana CASFETA kulijua Neno la Mungu kikamilifu na kulitenda huku akiwaambia kuwa silaha kuu ya kuangusha ngome ni kujikita zaidi katika maombi na kuwa na imani dhabiti.


Mwenyekiti wa Casfeta katika Mkoa wa Dar es Salaam, Samuel Nshatsi, alisema kuwa lengo la kukutana katika ibada hiyo ni kumsifu Mungu na kumwabudu ikiwa ni pamoja na kumlilia awanusuru vijana ambao bado wanazidi kutumikishwa na shetani.

Mbali na hilo, alisema kuwa moja ya malengo yao makubwa ni kuhakikisha wanatekeleza  kauli mbiu yao ya Mpango Mkakati, Mpango Shughuli na Mpango Kazi, kama dira ya vipaumbele ndani ya mwaka huu katika kumtumikia Mungu na kuhakikisha mabadiliko yanapatikana kwa viwango vya juu.

Aidha hakusita kutoa wito kwa vijana wa Tanzania, ambapo aliwataka wamkimblie Kristo na kuachana na dunia na kusemakuwa hali hivi sasa ni mbaya,  huku akibainisha kuwa shetani yuko kazini akimuwinda kijana. 

No comments:

Post a Comment