Mch. Dar kukabiliana na mafundisho potofu.

Akemea wanaotukuza kundi la Freeemasons, aelezea fursa sahihi za kubarikiwa na kufanikiwa.

Kutokana na kuibuka kwa wimbi kubwa la mafundisho yenye kupotoa imani, kupitia njia mbalimbali vikiwemo vyombo kadhaa vya habari, Mchungaji Ron Swai wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God, Dar es Salaam Calvary Temple (DCT), amejitolea kukabiliana na mfumuko huo.

Mchungaji Swai, alibainisha hayo siku chache zilizopita kanisani kwake, wakati wa ibada maalum ambapo alibainisha kuwa, katika nyakati hizi za mwisho, kuna kundi la watu ambao aidha kwa kutokujua Neno la Mungu kwa usahihi, ama kwa makusudi, wamekuwa wakitumia vyombo vya habari kupotoa maandiko na kuwahadaa watu kwa matangazo yao ya baraka.

Mchungaji Ron Swai wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God, Dar es Salaam Calvary Temple (DCT)

“Niko radhi kupambana na mafundisho potofu yanayotolewa na baadhi ya watu kupitia vyombo mbalimbali vya habari, nitatoa mafundisho yatakayowatoa watu kwenye mtazamo hasi na kuwarejesha katika msingi imara wa kufahamu Neno la Mungu na kuliishia,” alisema Mchungaji huyo na kuongeza:

“Yameibuka mafundisho mengi yenye falsafa potofu ambayo mtu akibarikiwa kwa wakati huu anasemwa kuwa amejiunga na Freemason, akikosa wanamwita akaombewe, ili abarikiwe, lengo ni kuwachanganya watu ili wasielewe Neno sahihi la Mungu.”

Aidha Mchungaji Swai, aliwataka watu kuondokana na dhana hiyo potofu, badala yake walisome Neno la Mungu, kwa usahihi, waliishi na kutekeleza yote yaliyoelekezwa humo ili wapate Baraka ambazo ziliahidiwa na ziko tayari kwa yule anayeamini.

Mtumishi huyo wa Mungu alisema atahakikisha anatumia vyema madhabahu takatifu ya Mungu kuhubiri, kufundisha kwa usahihi Neno, bila kupindisha ili kubadilisha mwelekeo wa falsafa potofu iliyogandamana ndani ya mioyo ya watu wengi walioumizwa.

Mbali na hilo Mchungaji huyo alisema, ameamua kufundisha somo hilo linalohusu kanuni sahihi ya kubarikiwa kwa mtu wa Mungu, baada ya kukutana na watu wengi walioumizwa na mafundisho potofu waliofika katika Kanisa la DCT kuomba msaada.

Aidha Mchungaji Ron, aliwataka watu kuelewe kwamba, kabla ya vitu vyote, Freemasons na mambo mengine Mungu alikuwepo na aliishatoa ahadi kwa wamchao, na kuwa jambo kubwa kwa sasa ni kuingia kwenye utekelezaji wa kumdai Mungu na sio kukimbilia ibada za maombezi ambazo mifumo yake inafanana sana na uganga wa kienyeji.

“Nasema Freemasons sio kila kitu, Mungu ni zaidi ya Free masons, watu wamefikia mahali hawamchi Mungu wa kweli, badala yake wanatoa heshima na utukufu kwa vitu vusivyofaa kabisa,” alisisitiza Mchungaji Swai

Mchungaji Ron, alikemea vikali tabia ya watu wanaojiita watumishi wa Mungu na kutumia vibaya mimbari kuwahadaa watu kwa utabiri wao kwa lengo la kujipatia pesa.

“Nasema achana kabisa na mambo hayo, umtukuze Mungu wa kweli ili upate Baraka zake zisizokuwa na majuto,” alisisitiza Mchungaji Ron.

No comments:

Post a Comment