Askofu Mtenga amtwisha Mkuu wa wilaya ujumbe mzito

 Askofu Mkuu wa Kanisa katoliki Jimbo Kuu la Songea, Nobert  Mtega amevitaka vyombo vyenye mamlaka serikalini kuacha mchezo wa kutumia silaha kali ovyo, kwa kuwa kufanya hivyo ni kuchochea machafuko na kuwaumiza watu wasio na hatia, hasa watoto na wakina mama.

Kauli hiyo aliitoa siku chache zilizopita wakati wa sherehe za shirika linaloshughulikia watoto waishio katika mazingira magumu na wanawake wanaojifunza ujasiriamali  la DMI,  mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Songea, Bw. Joseph Mkirikiti.

Askofu Mkuu wa Kanisa katoliki Jimbo Kuu la Songea, Nobert  Mtega
Alisema mahali popote  ambapo machafuko yapo,  yalianza kidogo kidogo na waathirika wakubwa ni watoto na wakina mama kwa kuwa kundi hilo, lina uwezo mdogo wa kujitetea na kuwafanya waangamie bila sababu za msingi.

"Watoto hawana walinzi zaidi ya sisi wenyewe,na  inatakiwa kutambua kuwa taifa bila watoto bado halijakamilika. Wao ni sehemu ya msingi katika jamii yoyote ile," alisema Askofu Mtega na kuongeza:

"Nawaambieni kama tutaachilia mambo haya ya kutumia silaha ovyo, yakaendelea kwa kweli tutakuwa tunatafuta machafuko ambayo yatahatarisha maisha ya watu wasio na hatia kabisa.”

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Bw. Joseph Mkirikiti.
Mtega alisema kinachoumiza zaidi wanaopatwa na athari za milipuko ya silaha hizo ni watu wasio na hatia,   badala yake   watu wa kuwajibishwa wanaachwa huru, jambo alilobainisha kwamba ni dhambi mbele za Mungu.

Mtumishi huyo wa   kanisa Katoliki alisema kuwa  kutumia silaha ovyo dhidi ya binadamu tena kwa yule asiyekuwa na hatia ni jambo la kishetani ambalo halistahili hata kidogo kwa kuwa linaweza kumkaribisha shetani katika jamii husika.

Kwa upande mwingine Mkuu  wa  Wilaya  ya Songea, Bw. Joseph Mkirikiti aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa shughuli hiyo alilipongeza shirika hilo kwa kazi nzuri ya kuwahudumia watoto waishio katika mazingira magumu, huku akiyaomba mashirika mengine kuiga mfano huo.

Mbali na hilo,  alichanganua kwamba jambo la msingi la kuangalia kwa makini ni eneo lililokosewa katika kumlea mtoto ikiwa ni pamoja na kufanya kazi ya kudumisha amani iliyopo ili vizazi viendelee kuwa na neema ya mafanikio.

No comments:

Post a Comment