Jengo jipya la ibada la kisasa lazinduliwa Zanzibar

Baada ya kuchomwa moto Kwa Kanisa la Elim Pentekoste, na watu wasiojulikana katika maeneo ya Kipange kisiwani Zanzibar, hatimaye jengo la kisasa lililogharimu shilingi milioni 35 limejengwa na kanisa hilo ili watu waweze kumwabudu Bwana.

Uzinduzi huo ulifanyika hivi karibuni visiwani humo, kufuatia kuchomwa moto kwa kanisa hilo, na watu wasiojulikana ingawa inadhaniwa kuwa ni waislamu wenye misimamo mikali.

Akihubiri katika uzinduzi wa jengo hio, lililochukua takriban miaka miwili, Askofu Peter Konki wa kanisa hilo, alisema ni lazima kujenga madhabahu iliyoanguka, huku akibainisha kwamba hakuna ibada yoyote itakayofanyika pasipo madhabahu.

“Jambo la muhimu kabla ya yote ni kujenga madhabahu, huo ndio moyo, kama moyo wa mtu hauko sawa sawa ibada ya nje haitakuwa salama, hata kama una jengo zuri namna gani,” alisema Askofu Konki.
Alisema madhabahu ya moyoni ni chanzo cha ibada zote, hivyo basi kama madhabahu ya moyoni imeanguka ibada yote ya nje itakuwa ni dhaifu na ya kimwili.

Mbali na hilo alisema pamoja na jengo hilo zuri lililogharimu zaidi ya milioni 35, halitakuwa na maana kama madhabahu ya mioyo ya watu imebomoka.
Hata hivyo aliwataka waumini wa kanisa hilo kuendelea mbele katika kumtetea Bwana Yesu na kusimama katika imani ili Mungu aweze kuokoa na injili kuhubiriwa katika kisiwa hicho.

No comments:

Post a Comment