‘Udini, ukabila ni hatari katika taifa’

Imeelezwa kuwa moja ya vitu hatari katika taifa lolote duniani vinavyoweza kuleta matatizo makubwa na mgawanyiko katika nchi, ni pale udini, ukabila na ubaguzi unapopewa nafasi kubwa pasipo kujua na kutambua madhara yake.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Naibu Msajili wa vyama vya siasa nchini Bw. Rajabu Juma jijini Dar es Salaam katika ofisi za msajili nchini.

Msajili huyo alibainisha kuwa kumekuwa na vuguvugu la udini, hivyo kuvitaka vyama vya siasa nchini kuepuka kujiingiza katika ubaguzi wa kidini na ukabila, huku akivitaka vyama vya siasa kuendesha siasa safi na zisizo na ubaguzi wa aina yoyote kwa maslahi ya taifa.


Aliongeza kuwa Tanzania itaendelea kuwa nchi  ya aman, ina utulivu pale wanasiasa watakapoendesha siasa zisizo na uchochezi wa aina yoyote pamoja na  kuepuka ubaguzi wa kikabila na udini huku wakimhusisha Mungu katika siasa zao, kwa lengo la kuleta maendeleo na mabadiliko katika taifa.

“Nchi yetu itazidi kuwa ya amani na utulivu kama wanasiasa watatambua wajibu wao, na si kuleta mgawanyiko katika taifa na kuendesha siasa chafu, hata vyama ambavyo vimepata usajili hivi karibuni viweze kufikia malengo yao vinatakiwa kutambua wajibu wao ili kufikia mafanikio,” alisema.

Hata hivyo hakusita kuvitaka vyama vipya vilivyosajiliwa karibuni kufuata sheria kanuni na taratibu za nchi, ikiwa ni pamoja na kutii sheria ya vyama vya siasa,  kwa lengo la kuepuka usumbufu wa aina yoyote unaoweza kujitokeza endapo watashindwa kutekeleza yale yanayotakiwa kutekelezwa.

Alizungumzia mfano Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), kimepata usajili wao kudumu hivi mara baada ya kutimiza masharti yote yanayotakiwa kutimizwa na chama chochote ili kupata usajili wa kudumu, ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kupata wanachama wa kutosha katika mikoa kumi nchini, ambapo kilipata zaidi ya watu 200, kila mkoa hivyo kuwa na sifa ya kupata usajili wa kudumu.

Saidi Miraji ni Mwenyekiti wa chama hicho kipya, ambapo mara baada ya usajili huo alipata nafasi ya kuzungumza na kusema kuwa chama chake kitakuwa tayari kufuata kanuni taratibu na sheria za nchi, huku akisisitiza kuwa hawatakuwa tayari kuendesha siasa za kuivuruga nchi bali kuleta mabadiliko katika taifa la Tanzania.
“Naamini kwamba kwa msaada wa Mungu tutayatekeleza yote ambayo tumeambiwa na msajili, chama hiki hakitakuwa na udini,ukabila wala  ubaguzi wa aina yoyote, kitakuwa na lengo moja la kuhakikisha kinaleta mabadiliko kwa taifa zima la Tanzania,” alisema Mwenyekiti huyo.

No comments:

Post a Comment