Kanisa la Anglikana latoa tamko dhidi ya waasi.

Kanisa la Angalikana nchini, limelitaka kundi la waasi la Kanisa la Watakatifu Wote la Mjini Sumbawanga linalokataa kumtambua Askofu wa Kanuni ya Dayosisi ya Lake Rukwa, Mathayo Kasagara, kukabidhi mali zote kwa wadhamini wa kanisa hilo vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Kauli hiyo iliyotolewa jana mjini hapa, inakuja siku chache baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk Valentino Mokiwa, kunusurika kupigwa na waumini wa kanisa hilo katika ibada iliyofanyika Septemba 23, kanisani hapo.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dk Valentino Mokiwa
Vurugu hizo zilitokea wakati kundi hilo linapinga uamuzi wa nyumba ya Maaskofu wa kumtambua Askofu Kasagara kuwa ni askofu wa Kanuni wa Dayosisi ya Lake Rukwa uliosomwa kwao na Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dk. Dickson Chilongani, mbele ya Askofu Dk Mokiwa na Askofu wa Dayosisi ya Ruaha, Dk Joseph Mgomi, ndani ya Kanisa la Watakatifu Wote.

Akisoma tamko hilo ambalo lilitokana na mkutano uliofanyika katika eneo la Mitumba mjini hapa Septemba 26, mwaka huu, Dk. Chilongani, alilitaka kundi hilo kuwasiliana naye na kukabidhi mali zote kwa wadhamini wa kanisa hilo.

“Viongozi wa kundi hili la waumini wanatakiwa wawasiliane na Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania ili wafanye utaratibu wa kukabidhi mali zote za Dayosisi ya Lake Rukwa kwa wadhamini wa kanisa Anglikana Tanzania kama zilivyoorodheshwa kwenye makubaliano yao na mahakama ambayo walitia saini.”alisema na kuongeza kuwa;

“Mali hizo ni pamoja na Kanisa la Watakatifu Wote, Ofisi ya Mchungaji, nyumba mbili za wachungaji, uwanja wa Kantalamba ulio na nyumba ya Askofu na Chapel ya Askofu, jengo la ofisi ambalo halijakamilika, viwanja 14 vya kanisa vilivyopo eneo la Majumba Sita pamoja na St. Mathias English Medium School.”

Aidha, Dk. Chilongani alisema nyumba ya maaskofu inalitaka kundi hilo la wakristo wanaompinga Askofu Kasagara waelewe kwamba muumini kuwa Mwanglikana ni suala la hiari na kama hakubaliani na mafundisho ya kanisa na maamuzi ya maaskofu amejitenga yeye mwenyewe na kanisa.

Akizungumzia mkutano huo wa maaskofu wa kanisa hilo uliofanyika mwishoni mwa mwezi Septemba, mwaka huu, Katibu huyo alisema kulingana na Katiba ya kanisa Anglikana Tanzania ya mwaka 1970 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004, kifungu cha 14 (8) Nyumba Ya Maaskofu imeridhika kabisa kwamba Askofu Kasagara ni Askofu halali wa Dayosisi ya Lake Rukwa.

Alikinukuu kifungu hicho kinachosema “Matokeo ya uchaguzi huo ni ya mwisho, hayatapingwa popote na taratibu za kumweka wakfu na kumsimika Askofu Mteule zitafuata.”

Alisema masuala ya uchaguzi wa askofu hayawezi kupelekwa katika mahakama za kidunia. Anayefanya hivyo au anayekusudia kufanya hivyo, kama ni Mkristo au Mhudumu anavunja Katiba ya Kanisa Anglikana Tanzania.

Kwa mujibu wa Katibu huyo, kundi hilo la waumini hao linalowakilishwa na Fulgence Rusunzu na Rojas Bendera ambao wanajitambulisha kuwa ni viongozi wa Kamati ya Usimamizi wa Kanisa la Watakatifu Wote katika mji wa Sumbawanga wamekuwa wakiandika barua kwa niaba ya Kamati kuwa wamekataa kumtambua Askofu Mathayo Kasagara.

Alisema hiyo ilikwishatoa uamuzi wake uliomo kwenye Deed of Settlement uliokubaliwa na pande zote mbili mbele ya Hakimu Mkazi M. W. Goroba Januari 17, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment