Mchungaji Msigwa aendelea kuibana wizara Maliasili na Utalii

Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa, amesema wizi wa pembe za ndovu pamoja na kuuliwa kwa wanyama, ni matokeo ya idara hiyo kuendelea kuwalinda majangili badala ya kuwachukulia hatua.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mchungaji Msigwa, alisema Rais Jakaya Kikwete, anatakiwa kuingilia kati na kuvunja mtandao wa ujangili ili kunusuru wanyamapori na maliasili nyingine za Taifa.

Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), alisema mpaka sasa ni miezi mitatu tangu alipowasilisha taarifa za ujangili bungeni na kumtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, achukue hatua dhidi ya majangili hao na matokeo yake amewajibisha watu watatu wa Idara ya Wanyamapori huku watuhumiwa wakubwa wakiachwa.
Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa


Alisema jambo hilo ni hatari na kusababisha idadi ya wanyama kupungua kila wakati.

Alisema wiki iliyopita, pembe za ndovu zenye uzito wa tani nne kutoka Tanzania na Kenya zenye thamani ya Sh. bilioni 2.5, ziliripotiwa kukamatwa na vyombo vya usalama vya mamlaka ya Jiji la Hong Kong.

Mchungaji Msigwa alisema tangu kutokea kwa tukio hilo mpaka sasa, waziri husika amekaa kimya pamoja na serikali yake juu ya suala hilo kana kwamba kilichotokea ni jambo la kawaida.

"Kama ilivyokuwa katika sakata la ununuzi wa rada, ni vema Watanzania wakazingatia kuwa hatua ya pembe za ndovu za Tanzania kukamatwa na vyombo vya usalama vya Hong Kong, ni kielelezo cha kuwa waziri na serikali wameshindwa hata kusimamia na kulinda maliasili zetu na kuviachia vyombo vya usalama vya nchi nyingine vikitufanyia kazi hiyo. Hii ni aibu kubwa kwa serikali na CCM," alisema.

Alisema pembe za ndovu zilizokamatwa ni matokeo ya kuendelea kuwalinda watuhumiwa wakuu wa ujangili.

Alikumbusha kwamba katika Mkutano wa Bunge uliopita, Kambi ya Upinzani bungeni pamoja na maoni ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliwataja vinara wa ujangili.

Alisema inashangaza kuona kwamba, hadi sasa watu hao hawajakamatwa hali inayochochea vitendo hivyo, wizi na ufujaji wa rasilimali nyingine za taifa.

"Kati ya wanaohutuhumiwa kuwa majangili, baadhi yao wameteuliwa katika Nec na pia ni washauri wa mwenyekiti wao. Hii ni hatari haina haja niwatajie majina wanajulikana na nyie fanyeni uchunguzi wenu mtawajua," alisema.

Alisema hatua za msingi zinatakiwa kuchukuliwa ili kutokomeza suala hilo katika kulinda utalii wa nchi pamoja na kuongeza uchumi wa nchi kupitia sekta hiyo.

Alidai Baloshingwa anafadhili pia majangili wanaoua wanyama katika mapori ya akiba ya Ugalla, Rungwe, Moyowosi na Maswa.

Alisema inashangaza kwamba wafadhili na majangili wanafahamika kwa majina, lakini hawachukuliwi hatua na pindi wanapokamatwa hufunguliwa kesi rahisi zenye dhamana hivyo huachiwa kwa dhamana.

"Usalama wa tembo uko hatarini kutokana na serikali kutochukua hatua dhidi ya ujangili wa tembo pamoja na taarifa hizi kuwepo serikalini na viongozi wa CCM kushiriki katika ujangili," alisema.

Tuhuma za Msigwa zinakuja wakati ambao Waziri Kagasheki amekuwa akisafisha Idara ya Wanyamapori ikiwemo kuwasimamisha vigogo wa idara hiyo.

Katika tukio la karibuni, Balozi Kagasheki amewatimua kazi vigogo watatu wa wizara hiyo akiwamo Mkurugenzi wa Wanyamapori, baada ya kubainika kuhusika katika kashfa ya utoroshaji wanyamapori hai kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwenda nje.

Vigogo hao wamefukuzwa kazi baada ya tume iliyoundwa kuchunguza kadhia hiyo kufanya uchunguzi na kumaliza kazi yake.

Katika kashfa hiyo, vigogo hao wanadaiwa kuhusika na usafirishaji wa wanyamapori hai 116 na ndege 16 Novemba 24 mwaka 2010,  kwenda nje ya nchi kupitia Kia.

Pia alisema biashara ya mkaa na hususani unaotokana na uvunaji wa misitu ya Pwani inafanywa kwa mtandao wa vigogo wa Idara ya Misitu ambao wameweka vijana kwenye kambi kwenye misitu hiyo.

"Na leo halitapita lori la mkaa kabisa kwa sababu vigogo walioandaa ziara hii wanajua kamati ya Bunge inakuja, wanazuia magari yao...hii ni biashara inayofanyika kwa mtandao kutoka wizarani, ukikamata lori simu zinapigwa na wanatoka ofisini kuja kuliruhusu liondoke," alisema.

Awali, akitoa taarifa ya hali ya misitu hiyo, Meneja Msaidizi wa TFS, Kanda ya Mashariki, Bernadetha Kadala, alisema hali ya misitu hiyo ni mbaya kwa kuwa imevamiwa na kuvunwa na wafanyabiashara haramu wa mkaa, kuni, mbao, kurunge na nguzo.

Alisema misitu hiyo pia imevamiwa na watu kwa ajili ya makazi na kilimo, na malisho ya mifugo.

"Maeneo mengi ndani ya misitu ya Ruvu yana uwazi kutokana na uharibifu huu," alisema.

Hata hivyo, alisema kumekuwa na doria za mara kwa mara ambazo zimewezesha kukamatwa kwa mbao, mkaa, kuni, nguzo, magogo, magari, pikipiki na baiskeli za wahalifu.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2012/13, doria zilizofanyika zimekamata malori matano, mkaa magunia 810, mbao 445, nguzo 150 na magogo 190.

No comments:

Post a Comment