Mbunge akusanya wachungaji kambini kushughulikia wachawi.

Kama ilivyokuwa enzi za Biblia, wakati wafalme walipokabiliwa na changamoto kubwa huwaita watumishi wa Mungu kuleta suluhisho, Mbunge wa Jimbo la Rorya mkoani Mara, Mh. Lameck Airo (CCM) ameamua kuwaalika watumishi wa Mungu, katika kambi maalumu ya wiki nzima ili kupambana na nguvu za giza zinazoleta maangamizi ya watu wasiokuwa na hatia jimboni kwake.

Akiongea na chazno kimoja cha habari hivi karibuni katika mahojiano Maalumu, Alhamisi iliyopita, Mhe. Airo alisema, amefikia uamuzi huo baada ya kugundua ukubwa wa tatizo la watu kulogana na kisha kujengeana chuki, katika kijiji cha Nyambogo, Kata ya kitembe, kitongoji cha Dagopa.

Huku akionenaka kuguswa na tatizo hilo, Mbunge huyo alisema: “Kumekuwa na vifo vinavyotokea katika mazingira tatanishi, watu hunyofolewa viungo vyao vya siri, na maiti zao kutupwa hovyo vichakani. Nimewasihi watu wangu kwa huruma za Mungu kuacha ushirikina na kumgeukia Mungu. Wachawi waache tabia hizo kwa kuwa zinasababisha mateso hata kwa familia zao.”

Mbunge wa Jimbo la Rorya mkoani Mara, Mh. Lameck Airo (CCM)
Alisema kuwa ujumbe huo aliotoa hadharani kijijini hapo, katika mkutano wa hadhara uliandaliwa na Diwani wa kata ya kitembe, Bw. Thomas Patrick ambaye wamekuwa wakishirikiana vyema katika kuwatumikia wananchi.

Kiongozi huyo, alisema ameamua kuwaita wachungaji na kuwakusanya kambini wakae huko kwa siku saba, wakipambana na roho ya uchawi na ushirikina kwa kuwa njia zingine zote haziwezi kuleta suluhisho la kweli.

“Nitagharamia kambi hiyo mimi kwa fedha zangu, na bado natoa wito kwa wachungaji wengine walio na utayari kuja katika pambano hili la kiroho tuwasiliane ili waingie kambini tukabili roho hii ya ulozi ambayo imekuwa ikitesa wananchi,” alisema Mbunge huyo.

Alisema kambi hiyo ya aina yake itafanyika Oktoba mwaka huu na tayari wachungaji wameshaanza kuonesha utayari wao wa kushiriki katika kambi hiyo kwa kuorodhesha majina yao.

Kama sehemu ya wapambanaji, waimbaji wa nyimbo za injili waliosimama pia wamealikwa ili kushiriki katika mapambano hayo.

Miongoni mwa watumishi wa Mungu walioguswa na mualiko huo na kueleza kuwa na utayari wa kwenda kwenye mapambano mstari wa mbele ni; Rev. Obeth Kyando wa Kanisa la EAGT, Geita, mkoani Geita ambaye alikiambia chanzo cha habari.


Mbunge wa Jimbo la Rorya mkoani Mara, Mh. Lameck Airo akiwa na waziri mkuu Mhe Pinda
 “Nimeitwa na Yesu nikatengwa na mambo mengine, hivyo niko tayari wakati wowote kwenda huko kulepeleka ukombozi mkuu. Nitakwenda pamoja na timu ya wanamaombi kutoka Geita na lazima kieleweke.”

Mchungaji mwingine aliyeeleza utayari wake katika mapambano hayo ni Swila Samson Swilla  wa Kanisa la TAG, Msasani jijini Dar es Salaam, ambaye alisema ameitwa kumtumikia Kristo na yuko tayari kwenda mahali popote kutekeleza wajibu wa wito wake.

No comments:

Post a Comment