Wenye fedha chafu wanapandikiza chuki ndani ya kanisa; Askofu Mokiwa

Askofu wa Kanisa la  Kianglikana nchini, Dk. Valentine Mokiwa,  amewataka watendaji wa kanisa hilo   kuwa macho na baadhi ya watu wenye uwezo mkubwa kifedha kupandikiza chuki  ndani ya madhehebu hayo.

Akizungumza  na waumini wa kanisa  hilo Dayosisi ya Mount Kilimanjaro,wakati wa ibada ya shukrani  baada ya kumalizika kwa mgogoro  uliokuwa unaikumba kanisa hilo,  Dk. Mokiwa alisema imeibuka tabia kwa baadhi ya viongozi wa kanisa kuogopa  kuwakemea watu wenye uwezo  mkubwa kifedha  hata kama wanakiuka sheria za kanisa.

Aidha, kiongozi huyo  pia amewataka  watendaji  wa kanisa hilo kutokubali  kupokea fedha za muumini  yeyote zitakazobainika kuwa hazikupatikana kihalali.

Dk.Valentine Mokiwa
 “Ni vyema  kutafuta fedha kwa bidii ili kupambana na umaskini na sio dhambi mtu kuwa fedha nyingi lakini ni dhambi kutafuta fedha kwa njia zisizo halali na ni vibaya zaidi kutumia fedha hizo  kupandikiza chuki mahali popote  ikiwemo  ndani ya kanisa” alisema askofu  Mokiwa na kuongeza:

“Itakuwa dhambi kubwa kwa viongozi  wa madhehebu ya dini  kuwatetemekea  na kuwaweka mbele watu wenye fedha na kushindwa kuwakemea pale wanapokwenda kinyume  na kufanya hivyo ni kwenda kinyume  na maelekezo  ya kanisa na maelekezo  ya Mungu.”


 Askofu Mokiwa pia amewaonya waumini  wanaodhani kuwa kwa kutumia fedha zao  watapata nafasi  ya  kuyavuruga madhehebu ya dini na kuwataka viongozi wa madhehebu ya dini  kuwa macho na makundi  ya  watu   wa  aina hiyo ambayo  amedai yamekuwa yakiongezeka siku hadi  siku.

Akizungumza katika ibada hiyo, Askofu  wa Dayosisi ya Mlima Kilimanjaro  Stanele Hotay, pamoja na kuwashukuru waumini wa kanisa hilo kwa mshikamano walioonyesha wakati  wote wa mgogoro, aliwawataka kuendeleza msimamo huo.

Aidha, Askofu huyo  ameiomba serikali  kuendelea kushirikiana kwa karibu na viongozi  wa madhehebu ya dini katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kukabiliana na umaskini  unaoendelea kuikabili  jamii.

Wakiwasilisha salam za serikali, Mkuu   wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo  na Mkuu wa Mkoa  wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, walisema serikali  itaendelea kushirikiana na viongozi  wa madhehebu ya dini  na kuhakikisha  kuwa uhuru wa kuabudu  unadumishwa kwa mwananchi  wote.

Dk. Nchimbi  amewataka  waumini  wa madhehebu ya dini  wanaopambana na viongozi  wao  kuacha mara moja utaratibu huo  kwani  licha ya kuwa hauna tija utawasababishia kupata laana  toka kwa Mungu.

No comments:

Post a Comment