Serikali yapiga marufuku Mihadhara ya Dini Nchini.

Serikali imepiga marufuku mihadhara yote inayochochea vurugu za kidini na kutangaza kuwakamata wote wanaofadhili vikundi hivyo.

Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi  wakati akizungumza na waandishi wa habari jana, jijini Dar es Salaam.

Alikuwa akizungumzia matukio ya vurugu zilizofanywa na baadhi ya watu wanaoaminika kuwa Waislamu katika miji ya Zanzibar na Dar es Salaam, yaliyotokea  juzi.

Alisema mihadhara yote ya kidini imepigwa marufuku kwa muda wa mwezi mmoja huku serikali ikifanya  uchunguzi ili kubaini watu wanaofadhili vurugu hizo kutoka nje na ndani ya nchi.

Dk. Nchimbi alisema Serikali imejipanga kuhakikisha inatumia nguvu pamoja na vyombo vya sheria endapo itabaini kuna dalili ya watu kufanya mipango ya kuanzisha vurugu kwa kisingizoa cha dini.

"Serikali tumechua maamuzi mapya kuhusu suala kama hili, hapo mwanzo tulikuwa tunawakamata wale wanaoshiriki lakini sasa tutawakamata wale wote waliofanikisha, waliotekeleza na waliowatuma," alisema waziri Dk. Nchimbi.

Alisema uamuzi huo wa Serikali umechukuliwa kwa nia njema ya kutetea nchi isitumbukizwe katika vita vya kidini na watu wachache ambao aliwaita ni wahuni.

Alisema chanzo cha vurugu zilizofanyika Zanzibar na Dar es salaam hazina msingi wowote kwa sababu madai yaliyotolewa na watu wa Kikundi cha Uamsho kwa Zanzibar na Jumuiya za Taasisi za Kiislamu  kwa Tanzania bara hazina msingi na Serikali hausiki.

No comments:

Post a Comment