Magari ya Wakristo yachomwa Tunduru.

Umoja wa Makanisa Tunduru mkoani Ruvuma, umeeleza kusikitishwa na mashambulizi yasiyokoma   yanayofanywa dhidi ya Wakristo na mali zao, kiasi cha kuwalazimu kuishi kwa hofu kubwa, huku wakilazimika kulala nje kujilinda  bila mafanikio.

Katika matukio ya karibuni kabisa magari mawili ya wakristo yaliteketezwa kwa moto yakiwa yameegeshwa nje ya nyumba zao, na inaaminika kuwa hiyo ni sehemu ya muendelezo wa mashambulizi dhidi ya Wakristo na mali zao.

Magari hayo yaliyochomwa usiku moja likiwa ni mali ya  Mchungaji Milinga wa Kanisa la KLPT, Tunduru  na Afisa ukaguzi Elimu, aliyejulikana kwa jina moja la Haule na matukio hayo bado yanachunguzwa na vyombo vya dola.

Katika tamko lao  kwa serikali, Umoja huo umeeleza mlolongo wa matukio ya kustaajabisha yanayofanywa dhidi yao, yakihatarisha usalama wa maisha yao na mali zao  na kuripotiwa Polisi lakini hakuna mtu aliyekamatwa  hadi sasa. Tamko hili lililokabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, limeorodhesha matukio kadhaa yakiwepo ya karibuni zaidi ya kuchomwa moto kwa magari mawili  ya Wakristo, moja likiwa la Mchungaji.

Katibu wa Umoja huo Fadha Mathias Mkapa,  wa kanisa Katoliki, akithibitisha kutoka kwa matukio hayo  alisema kuwa, kwa ujumla hali ni mbaya na wamelazimika kuonana na Mkuu wa Wilaya kumueleza masikitiko yao.

Katika tamko la  Umoja huo lililowasilishwa serikalini, Septemba 21, mwaka huu umoja huo umeorodhesha matukio yote yaliyotokea  katika eneo hilo na kutoa mapendekezo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuitaka serikali kupiga marufuku mihadhara yenye kukashfu  dini zingine.

Katika tamko hilo, umoja huo umeeleza kuwa matukio hayo ya kihalifu  yalianza Septemba  kwa kuchomwa kwa mabanda 5 ya nguruwe na  mali za Wakristo,

Saa chache kabla ya mashambulizi hayo, kulikuwa na mhadhara wa kiislamu hapa Tunduru ambao ulikuwa na matusi mengi kwa Wakristo na inaaminika kuwa kuna uhusiano na matukio kwa kuwa Waislamu wamegoma hata kushiriki  masuala ya ulinzi wakitoa masharti kwanza nguruwe na mbwa waondoshwe kabisa katika maeneo hayo kwani wao hawawezi kulinda mbwa na nguruwe.

Kutoka katika eneo la tukio, Mchungaji Emmanuel Ernest Kanduru, wa Kanisa la TAG –Tunduma , ambaye pia ni Mwangalizi wa Sehemu hiyo,  alisema kuwa, kabla ya kulipuka kwa mashambulizi hayo, aliandaa mkutano wa Injili na mhubiri mmoja kutoka jijini Dar es Salaam, alihubiri na watu wengi kuguswa, wakaachana na mambo ya dunia na kumpokea Yesu.

Kisha Mchungaji Kanduru aliongeza: “Kana kwamba hawakuridhika, kundi hilo la watu tunaodhani kuwa ni Waislamu wenye msimamo mkali walivamia mabanda matano ya nguruwe na kuyachoma moto usiku wa manane  ambapo nguruwe 40 walikufa hapo hapo na wengine 20 siku iliyofuata.

Matukio hayo yaliendelea tena usiku wa Septemba  18, ambapo  nyumba ya Mkristo aitwaye  Jastin Magwinda iliteketezwa kwa moto yeye na familia yake ya watu watatu walinusurika  kufa.

Tamko hili lilieleza kuwa baada ya tukio hilo, lilifuata tukio la kuchomwa moto kwa banda la nguruwe la Mchungaji Jacob Malanzi wa Kanisa la Biblia, lilichomwa moto na siku iliyofuata lilifanyika jaribio la kulipua mashine ya kusaga na kukoboa, hata hivyo lilizimwa kabla ya kuleta hasara kubwa.

“Tukio hilo lilifuatia lile la uchomaji wa banda la nguruwe la Padre Edwin Naka na kwa bahati, nguruwe walisalimika, lakini wakati Polisi wakishughulikia tukio hilo; waligundua shambulio lingine la moto, ambapo mabanda ya Bw. Mingoi yalikuwa yamelipuliwa kwa moto na wakahusika kuuzima, lakini pamoja na matukio yote hayo ya dhahiri hakuna tamko la serikali lililotolewa,” ilisema sehemu ya tamko hilo.
Kisha tamko likaendelea:

MIHADHARA
Katika tamko lao, viongozi wa Umoja wa makanisa Tunduru wameitaka serikali kusitisha mihadhara yote  yenye kuigusa imani nyingine na kuchochea chuki miongoni mwa jamii. Anayepewa kibali cha mkutano apewe sharti la kutogusa imani za wengine badala yake ahubiri imani yake tu, na wanaokufuru dini zingine washtakiwe mahakamani.

Aidha viongozi hao wameitaka serikali kutoa haki sawa kwa viongozi wa dini wanaoomba vibali vya mikutano ikiwa ni pamoja na muda wa kuanza na kumaliza, ili kuondoa malalamiko ya kuwepo kwa upendeleo.

Viongozi hao wa dini wameitaka serikali kuwalipa fidia wale wote walioathiriwa na machafuko hayo, kwa kuwa wengine hadi sasa wanalala nje na hawana hata mahali pa kujihifadhi.

Katika tamko hilo lililosainiwa na viongozi 19 wa madhehebu mbalimbali waliwataka viongozi wa Serikali na wale wa dini kufanya kazi pamoja katika kuhakikisha amani ya nchi inalindwa kwa gharama yeyote ile bila kujali dini flani.

No comments:

Post a Comment