Waimbaji wa muziki wa Injili waaswa.

Waimbaji wa muziki wa Injili nchini, wametakiwa kuimba nyimbo ambazo zina mafundisho ya kukemea na kufundisha jinsi ya kujiepusha na maambukizi ya ukimwi na matumizi ya dawa za kulevya.

Pia waimbaji wametakiwa kutunga nyimbo ambazo zina mafundisho sahihi katika jamii, kwa lengo la kuhakikisha panakuwepo na mabadiliko katika jamii, hususan vijana ambao wanakaa vijiweni na kutumia dawa za kulevya.

Rai hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Walk for Hope, Emmanuel Mbaule, alipokuwa akizungumza na waimbaji wa muziki wa Injili mjini yaani Dodoma.

Mbaule alisema kuwa, pamoja na kuwepo wimbi kubwa la waimbaji wa muziki wa Injili, lakini bado hawajafikia hatua ya kubadilisha tabia za watu hususan vijana, ambao wanakaa vijiweni kwa kujidunga sindano za dawa za kulevya.

Alisema matamasha ambayo yanakusudiwa kufanywa na waimbaji wa nyimbo za Injili ni nyimbo ambazo zina ujumbe wa moja kwa moja wa kukemea maambukizi ya ukimwi na uvutaji wa dawa za kulevya.

Mbali na hilo, Mbaula alisema tamasha hilo pia linakusudia kuhakikisha waimbaji wanatumia muziki wao kama sehemu ya kukuza uchumi badala ya kuimba nyimbo ambazo zinawanufaisha wengine.

Alisema inasikitisha kuona wapo baadhi ya waimbaji wa nyimbo za Injili wanakuwa masikini bila kutambua kuwa nyimbo zao ni mali kubwa.

“Huwezi kuimba nyimbo za Injili na ukaendelea kuwa maskini, nyimbo za Injili ni muhimu sana, kwani unakomboa roho za watu na kuwafanya wapate neema ya ufalme wa Mungu na wala si vinginevyo.

“Muziki uthaminiwe, kwani kwa kuimba unaweza kutengeneza ajira na kukuza uchumi wa mwimbaji, badala ya mtu kuzunguka na albamu yake bila mafanikio,” alisema Mbaule.

No comments:

Post a Comment